TRA Yatoa Utaratibu wa Kusajili Walipa Kodi Wadogo.
Kamishna wa Kodi za Ndani, Elijah
Mwandumbya (kulia)akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo
pichani) leo Jijini Dar es Salaam kuhusu uzinduzi wa Kampeni ya Usajili wa
Walipakodi.
Na mwandishi wetu
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeondoa
utaratibu wa awali kwa walipakodi wadogo kulipia kodi kabla ya kuanza kufanya
biashara na badala yake kuwataka kulipia robo ya kwanza ndani ya siku tisini
tangu kusajiliwa.
Kamishna wa Kodi za Ndani, Elijah Mwandumbya
ameyabainisha hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake
na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa Kampeni ya Usajili wa Walipakodi.
Mwandumbya amesema jukumu la usajili wa walipakodi kwa
Mamlaka hiyo ni chanzo cha kuongeza idadi ya walipakodi, wigo wa ulipaji kodi,
kuongeza makusanyo pamoja na kuwa na taarifa sahihi za walipakodi wanaostahili
kukadiriwa na kutozwa kodi ili kuchangia Pato la Taifa.
“kampeni hii inaenda sambamba na mabadiliko makubwa tuliyoyafanya
kwa walipakodi wadogo kwa kuwapa siku tisini za kulipa kodi kwa robo ya kwanza
ya malipo pindi tu watakapokuwa wamesajiliwa hivyo mabadiliko hayo yatakuwa
chachu katika usajili kwani tunatarajia kusajili walipakodi takribani milioni
moja nchi nzima,”alisema Mwandumbya.
Kamishna wa Kodi za Ndani amesisitiza kuwa usajili wa TIN ni bure
na utafanyika katika ofisi zote za Mamlaka hiyo na katika vituo maalum
vitakavyokuwa vimeteuliwa na kutangazwa kupitia vyombo vya habari na matangazo
katika maeneo husika.
Aidha, Mwandumbya amewataka wananchi kujihadhari na vishoka
wanaoweza kutumia mwanya wa kuharibu nia njema ya kampeni hiyo kwani hakuna
wakala yeyote aliyepewa jukumu la kusajili wala kutoa fomu za usajili wa zoezi
hilo.
Amefafanua kuwa muhusika lazima aende mwenyewe ili apigwe picha na
kuchukuliwa alama za vidole pia atatakiwa aende na mkataba wa pango au
uthibitisho wa umiliki wa mahali pa biashara, barua yenye muhuri na namba ya
simu ya Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa pamoja na kitambulisho cha muhusika
kama vile hati ya kusafiria, leseni ya udereva, kitambulisho cha uraia au cha
mpiga kura.
Kampeni hiyo imezinduliwa nchi nzima kwa nia ya kuhakikisha kila
mwananchi anayestahili kupatiwa namba ya utambulisho ya mlipakodi anasajiliwa
na kupata namba hiyo kwa urahisi na haraka.
No comments