Breaking News

Naibu Waziri nishati aagiza utekelezaji Rea III uanze haraka

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) akizungumza na baadhi ya wananchi wa Kata ya Ibanda (kulia) wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Wilayani Kyela.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) akimsikiliza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Kyela, Mhandisi Matei Mshana (kulia) alipofanya ziara kwenye Kituo cha Kuwashia na Kuzimia Umeme (Switch Yard) kilichopo katika Kata ya Nkuyu Wilayani humo.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) alipofanya ziara kwenye Bandari ya Itungi ya Wilayani Kyela ambayo ni moja ya maeneo yaliyonufaika na Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II). Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta na kulia ni Saleh Songoro ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd inayojenga Meli ya Abiria kwenye Bandari hiyo.

...............
Serikali imeagiza utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) uanze mwezi huu wa Januari, 2018 sambamba na utekelezaji wa Mradi wa Densification ambao upo kwenye utekelezaji.

Naibu Waziri Nishati, Subira Mgalu ametoa agizo hilo Januari 6, 2018 wakati wa ziara yake ya kutembelea maeneo mbalimbali ambayo Mradi wa Umeme Vijijini unatekelezwa Wilayani Kyela, Mkoani Mbeya.

Mgalu alizungumza na baadhi ya wananchi Wilayani humo ambao walimueleza kero mbalimbali zinazohusu masuala ya Nishati ya Umeme ambayo ni kukatika kwa umeme mara kwa mara bila taarifa, kucheleweshwa kuunganishwa na huduma ya umeme kwa ambao tayari wamelipia, baadhi ya Taasisi (shule, zahanati, vituo vya afya na visima vya maji) kurukwa wakati wa utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II).

Baada ya kuzungumza na wananchi hao kwa nyakati tofauti, akijibu kero zao, Naibu Waziri Mgalu aliagiza Mradi wa REA III uanze kutekelezwa ndani ya Mwezi huu wa januari, 2018 bila kuchelewa.

“Utekelezaji wa Mradi wa Densification ambao unafanyika hivi sasa, uende sambamba na utekelezaji wa Mradi wa REA III kuanzia Mwezi huu wa Januari, 2018,” aliagiza Mgalu. 

Akizungumzia suala la kucheleweshwa kuunganishwa na huduma ya umeme kwa wananchi waliolipia, Mgalu aliliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha wateja wote waliolipia umeme wanaunganishwa mara moja bila kuwepo visingizio.

“Tulikwisha agiza maombi yote ya wateja kuunganishiwa umeme yatekelezwe ndani ya Siku Saba baada ya kulipia,” alisema Naibu Waziri Mgalu.

Aidha, kuhusu suala la baadhi ya maeneo kurukwa hususan maeneo ya huduma za kijamii zikiwemo shule, zahanati, vituo vya afya na visima vya maji, Naibu Waziri Mgalu alisisitiza kwamba wakati wa utekelezaji wa Mradi huo wa REA III, maeneo hayo yapewe kipaumbele.

“Tunakiri utekelezaji wa REA II, ulikuwa na mapungufu ikiwemo ya kuruka baadhi ya maeneo, ninawahakikishia kasoro hii haitojirudia kwenye REA III,” alisema.

Aliongeza kuwa TANESCO itoe taarifa mapema kwa Wananchi kama kutakuwa na ukataji wa umeme kutokana na sababu mbalimbali na kwamba iongeze ubunifu katika utekelezaji wa shughuli zake ikiwemo kuwafuata wateja na kufungua Vituo maeneo ya Vijijini ili kuwarahisishia wananchi wa maeneo hayo upatikanaji wa huduma.

Aidha, baadhi ya maeneo ulikopita Mradi wa Umeme Vijijini wa REA aliyotembelea Naibu Waziri Mgalu katika ziara hiyo Wilayani Kyela ni Bandari ya Itungi; Kata ya Kajunjumele; Kata ya Nkuyu; Kata ya Ibanda na Kata ya Kasumulu.

Bandari ya Itungi ni mnufaika wa Mradi wa REA II ambapo baadhi ya shughuli zake hutekelezwa kwa kutumia Nishati ya Umeme ikiwemo shughuli inayoendelea hivi sasa ya Uundaji wa Meli ya abiria inayofanywa na Mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd.


Naibu Waziri Mgalu yupo Mkoani Mbeya kwa ajili ya ziara ya kukagua utekelezaji  Miradi ya Umeme Vijijini na Miradi mingine ya umeme Mkoani humo.

No comments