Breaking News

Mhe Mwanjelwa: maendeleo hayana mipaka ya vyama

 Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akishiriki ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari Iyera wakati akiwa ziarani Mkoani Mbeya, Jana 2 Januari 2018. 


 Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akikabidhi mifuko 20 ya saruji kwa ajili ya kuongeza nguvu katika ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya Sekondari Iyera wakati akiwa ziarani Mkoani Mbeya, Jana 2 Januari 2018.


Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akichanganya udongo wakati akishiriki ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari Iyera wakati akiwa ziarani Mkoani Mbeya, Jana 2 Januari 2018. Wengine (Kulia) aliyeshika jembe ni Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe Paul Ntinika na Kushoto ni Diwani wa Kata ya Iyera (CHADEMA) Mhe Charles Mkera.

Na Mwandishi wetu
Maendeleo ni mchakato wa kujenga jamii endelevu, yenye kujiamini,  kujituma na uwezo wa kushiriki, kwa misingi ya usawa na kuheshimiana, katika kubuni, kuandaa na kutekeleza mipango ya kujiletea “maendeleo” na kutumia matokeo ya kazi zao.


Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa amekuwa mwalimu mzuri wa somo la Uraia Mkoani Mbeya akifundisha kuhusu umoja na mshikamano huku akisisitiza kuwa Maendeleo ni dhana pana kwa wananchi na hayapaswi kufanywa kwa mipaka ya vyama vya siasa.


Mhe Mwanjelwa ameyasema hayo Jana 2 Januari 2018 wakati akizungumza na wananchi na mafundi wanaojenga majengo ya Shule ya Sekondari Iyera ili kutatua changamoto ya kuwa na vyumba vingi vya madarasa kwa ajili ya kuhimili wingi wa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.


Amewasisitiza mafundi hao kujenga madarasa hayo kwa haraka na viwango vya hali ya juu kwani shule zinatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni huku shule hiyo ikiwa na upungufu wa vyumba vinne vya madarasa.


Mhe Mwanjelwa alisema kuwa tangu serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kutangaza utoaji elimu bure kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi sekondari kumekuwa na ongezeko kubwa la wananfunzi wanaojiunga na masomo ikiwa ni pamoja na kurejea shuleni kwa wananafunzi waliokata tamaa ya kuendelea na masomo.


Alisifu juhudi za Uongozi wa Wilaya ya Mbeya kwa kushirikiana kwa pamoja na wananchi katika shughuli za maendeleo huku akiipongeza Halmashauri ya Jiji la Mbeya kwa kufanya vyema na hatimaye kuongoza kwa ufaulu wa wanafunzi dhidi ya Halmashauri zingine za Mkoa wa Mbeya.


Sambamba na hayo pia Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa ameongeza nguvu kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule hiyo ya Sekondari Iyera kwa kuchangia mifuko 20 ya saruji.

No comments