Breaking News

MWALIMU MBARONI KWA KUTUKANA FACEBOOK



JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mkolani, Deogratius Kisandu, akidaiwa kutumia lugha ya matusi, kejeli na kudhalilisha katika ukurasa wake wa Facebook.


Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema Kisandu alikamatwa jana baada ya kuwepo taarifa kuhusu kuonekana ujumbe wa matusi na lugha zisizofaa katika ukurasa wake wa Facebook.

Alisema walimfuatilia mtuhumiwa na kumkamata akiwa na simu yake ambayo huitumia kupeleka na kuandika matusi hayo kinyume na Sheria Namba 4 ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.

“Polisi bado wanaendelea na mahojiano na upelelezi dhidi ya mtuhumiwa. Utakapokamilika atafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.

“Taarifa zinaonyesha kuwa mtuhumiwa amewahi kushtakiwa kwa makosa kama hayo kipindi cha nyuma,” alisema Kamanda Msangi.

Kamanda amewataka vijana wanaotumia mitandao ya jamii kuacha kwa sababu ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi siku mbili zilizopita kuhusu lugha ya kudhalilisha, matusi na kejeli inayotumiwa na Kisandu ambaye pia ni mtumishi wa umma, katika ukurasa wake wa Facebook.
“Tumetumia siku mbili mpaka kumpata Kisandu. Mwanzoni nilifikiri labda haya mambo yanafanywa na mtu ambaye si raia wa Tanzania lakini katika mahojiano amekiri yeye ni Mtanzania.

“Kwa kweli lugha anayoitumia ni ya kudhalilisha, matusi na kejeli na haifai kutumiwa kutokana na utamaduni wetu,” alisema.

Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa, Lawi Odiero, alisema sheria ipo na inakataza matumizi mabaya ya mitandao na kwa kuwa kesi hiyo ipo polisi atatoa ushirikiano unaohitajika kusaidia uchunguzi.

No comments