KUHUSU WALIOFUKUZWA KWA VYETI FEKI, WENYE VYETI VYA DARASA LA 7
HATIMA ya mafao ya wafanyakazi wa serikali walioondolewa kwenye ajira
kutokana na kubainika kuwa na vyeti feki itajulikana kabla ya Bunge la
Bajeti, imefahamika.
Hatua hiyo inatokana na serikali kujibu hoja nane za Shirikisho la Vyama
vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) na kwamba suala la kulipwa au
kutolipwa haki zao litafahamika Machi au Aprili, mwaka huu.
Hoja zingine ni ajira ya waliomaliza darasa la saba, kupandishwa
madaraja, madeni ya wafanyakazi, nyongeza za mishahara, kutofanyika
vikao vya bodi, kujua idadi ya taasisi zilizoundwa na kuunganishwa kwa
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Katibu Mkuu wa Tucta, Dk. Yahya Msigwa, alisema jana jijini Dar es
Salaam kuwa mamlaka mbalimbali zinamalizia kulifanyia kazi suala la
vyeti feki na kwamba kabla ya Mei Mosi, mwaka huu, hatima yao itakuwa
imepatikana.
“Unajua kilichofanyika ni kosa la jinai na la kinidhamu, hivyo sisi
Tucta tunaendelea kuiomba serikali angalau wapatiwe kifuta machozi,”
alisema.
Alisema ajira kwa waliomaliza darasa la saba Serikali ilitoa waraka
unaosema watumishi wa umma wanapaswa kumaliza elimu ya kidato cha nne
kuanzia Mei, 20, 2004.
Pia alisema baada ya hapo, walitakiwa kujiendeleza ili kuwa na vigezo
vya kuendelea kuwa watumishi wa umma iwapo zipo baadhi ya idara
zinawahitaji na kujenga hoja.
Kuhusu kupandishwa madaraja,
Dk. Msigwa alisema watumishi wengi hawajapandishwa kutokana na uhakiki
wa vyeti, hivyo serikali imetenga fedha kwa ajili ya mpango huo kwa
kutegemea bajeti ijayo.
Alisema malipo yataanza tangu siku ya kupata barua ili kupunguza madeni
ambayo inadaiwa na kwamba kimsingi katika hilo, yako madeni ya mishahara
na isiyo ya mishahara.
Kuhusu madeni, kwa mujibu wa Dk. Msigwa, serikali imesema imemaliza
uhakiki na imeanza kulipa lakini itakuwa vigumu kulipa watu wote kwa
mkupuo bali watazingatia uhakiki ya madeni yenyewe.
Kwa upande wa nyongeza ya mishahara, alisema Rais John Magufuli
hakuahidi wakati wa sherehe za Mei Mosi bali nyongeza hiyo italolewa
mwaka huu.
Aidha, Dk. Msigwa alisema hoja ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya
jamii kuwa na mifuko miwili, mmoja wa binafsi na mwingine wa umma,
imetokana kauli za wafanyakazi wenyewe kwenye sherere za Mei Mosi.
Alisema rasimu iliyotegenezwa si mbaya licha upungufu uliopo na wanaendelea kutoa maoni kabla muswada haujawasilishwa Bungeni.
No comments