Breaking News

JKCI yaokoa milioni 800 kwa kufanyia upasuaji moyo watoto 20

1
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto ya nchini Israel na Kituo cha Moyo cha Berlin kutoka nchini Ujerumani wamefanya upasuaji wa moyo bila kufungua kwa watoto 15 kati ya watoto 20 wenye matatizo ya moyo waliopangwa kufanyiwa matibabu hayo.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Tiba JKCI, Dkt. Peter Kisenge amesema upasuaji huo unaotumia mtambo wa Cathlab umefanyika katika kambi maalumu ya matibabu iliyoanza Januari 20 ambayo inatarajiwa kumalizika kesho Januari 25, 2018, ambapo watoto 32 walifanyiwa uchunguzi wa moyo.

Amesema upasuaji wa watoto hao katika taasisi ya JKCI umeokoa zaidi ya milioni 800 ambazo zingetumika kuwasafirisha na kuwatibia wagonjwa nje ya nchi.

Dkt. Kisenge amesema matibabu mengine yaliyofanyika ni pamoja na kuzibua matundu kwenye moyo, kutanua mishipa ya moyo kwa watoto wenye umri kuanzia mwezi mmoja hadi miaka 18.

Matibabu hayo yamefanywa na Timu ya madaktari bingwa wa moyo kutoka taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto iliongozwa na Dkt. Sagi Assa na wa kituo cha Moyo cha Berlin kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa JKCI.

No comments