Kamanda Mambosasa awatembelea na kuwafariji askari Walioko Kibiti, Rufiji
Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imetembelea Mkoa wa Rufiji katika utaratibu wa
kawaida wa jeshi hilo wa kuimarisha ujirani mwema na kubadilishana uzoefu.
Makamanda
wa polisi wa mikoa inayounda Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wakiongozwa na
Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa walifika Mkoa wa Kipolisi wa Rufiji leo
Jumanne Januari 2,2018 na kupokewa na kamanda wa mkoa huo, Onesmo Lyanga.
Msafara
wa Kamanda Mambosasa ulibeba zawadi za sikukuu kwa ajili ya askari ambao wapo
katika operesheni maalumu katika eneo hilo ambalo siku za nyuma liligubikwa na
matukio ya mauaji ya wananchi wasio na hatia na askari.
Akizungumza
na baadhi ya askari waliopo Rufiji, Kamanda Mambosasa amewapongeza kwa kufanya
kazi kwa uzalendo na kwa kufuata kiapo chao licha ya mazingira ya kazi si
rafiki.
"Hakuna
asiyejua hali iliyokuwepo Rufiji mpaka wananchi wakakata tamaa na wengine
walihama lakini kamanda mwenzangu ameniambia hali sasa ni shwari, Dar es Salaam
tuko pamoja na ninyi na tunathamini kazi mnayoifanya. Usalama wa Dar es Salaam
unategemea kwa kiasi kikubwa usalama wa hapa pia," amesema Kamanda
Mambosasa.
Amesema
hali ya usalama Dar es Salaam ni shwari na askari hawajalala wapo imara kama
walio kwenye operesheni hiyo kwa kuwa wahalifu wanaobanwa Pwani na kukimbilia
Dar es Salaam hawabaki salama.
"Hatukuja
Boxing day (siku ya kufungua zawadi) lakini leo tumewaletea ndafu, kidogo, kilo
200 za mchele, sukari, maji na mafuta, ninyi endeleeni kupeperusha bendera ya
Jeshi la Polisi na haya mambo yatakwenda lakini baadaye yataisha,” amesema.
Kwa
upande wake, Kamanda Lyanga amesema wamekuwa wakitembelewa na viongozi na
watu wengine wengi, hivyo morali ya askari waliopo katika operesheni iko juu na
wanafanya kazi kwa weledi na mpaka sasa hakuna malalamiko yoyote ya wananchi
jambo ambalo linaashiria kuwa sheria zinafuatwa.
"Baada
ya kuwa tumewafikia wahalifu sasa wananchi wanawapenda askari wao, wanatoa
taarifa hawaogopi tena kama zamani," amesema Kamanda Lyanga.
No comments