Breaking News

DC SHINYANGA AUNGANA NA WANANCHI KUZUIA MAJI BWAWA LA MWALUKWA YASITOROKE


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro leo Ijumaa Januari 26,2018 ameungana na wananchi wa kijiji na kata ya Mwalukwa iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (Vijijini) kuziba ukingo wa bwawa la Mwalukwa ambao umebomoka na kusababisha maji yatoroke.

Matiro aliyekuwa ameambatana na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bahati Kasinyo Mohammed pamoja na baadhi watendaji wa halmashauri akiwemo Injinia wa maji Silvester Mpemba aliungana na wananchi kuziba sehemu ya ukuta/ukingo wa bwawa iliyobomoka na kusababisha maji yavuje/yatoroke.
Bwawa hilo lililojengwa kwa nguvu ya wananchi kati ya mwaka 1941- 1951 linahudumia wananchi wa kata ya Mwalukwa yenye vijiji vinne ambavyo ni Ng’hama,Bulambila,Mwalukwa na Kadoto B lakini pia kijiji cha Mwamadilanha kilichopo katika kata ya Pandagichiza.

Akizungumza wa zoezi hilo la kuziba sehemu ya bwawa inayovuja,Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro aliwataka wananchi kutunza bwawa hilo wakati serikali inaendelea na utaratibu wa kufikisha huduma ya maji ya mradi wa Ziwa Victoria katika vijiji ambavyo havijafikiwa na mradi huo.

“Nimekuja hapa kuungana nanyi kuongeza nguvu ya kuzuia maji yasitoke,niwapongeze pia kwa kuja,naomba mtunze bwawa hili kwani kuna maeneo mengine wanatamani kuwa na bwawa kama hili,maafisa watendaji ,viongozi wa sungusungu na viongozi ngazi za vijiji na kata wekeni utaratibu wa kutunza hili bwawa kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo yenu”,alisema Matiro.

Hata hivyo Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Bahati Mosinyo Mohamed alisema pesa zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo bado hazijafika hivyo kuwataka wananchi kutokuwa na hofu kuwa huenda pesa zimeliwa na baadhi ya watu.

Nao Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Ngelela na katibu wake Jumanne Katundu walioshiriki katika zoezi hilo,waliwaomba viongozi wa vijiji na kata kuunda sheria na kanuni kwa ajili ya kutunza bwawa hilo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro (wa tatu kushoto) akiangalia maji yaliyoroka katika bwawa la Mwalukwa lililopo katika kata ya Mwalukwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.Kulia ni wananchi wa kijiji cha Mwalukwa wakiweka mchanga kwenye mifuko ili kuzuia maji yasitoroke katika bwawa hilo.
Sehemu ya bwawa la Mwalukwa.
Kulia ni diwani wa kata ya Mwalukwa Ngassa Mboje akionesha sehemu ambayo bwawa limemong'onyoka ukuta na kusababisha maji yavuje/yatoroke.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akifukia sehemu ya ukingo wa bwawa hilo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro (kulia) akishirikiana na wananchi wa kijiji cha Mwalukwa kuchimba udongo kwa ajili kuziba sehemu ya ukuta/ukingo uliobomoka katika bwawa la Mwalukwa.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro (kulia) akiwa amebeba karai la udongo aliouchimba kwa ajili ya kuziba ukingo/ukuta wa bwawa la Mwalukwa.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akishirikiana na mwananchi kubeba mfuko wa udongo kwa ajili ya kuziba ukuta wa bwawa la Mwalukwa.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwasititiza wananchi kulinda bwawa hilo.

No comments