Breaking News

WAZIRI MKUU AFUNGUA MAKUCHA BUTIAMA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Takukuru imkamate na kumhoji meneja wa mkoa wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Peter Salim baada ya kushindwa kutekeleza ujenzi wa mradi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.


Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu imesema mtendaji huyo mkuu wa Serikali alisema licha ya Serikali kutoa Sh600 milioni Aprili mwaka jana kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi hizo, hadi sasa hakuna kilichofanyika.


Hata hivyo, meneja huyo katika alisema maelezo yake alieleza kuwa hadi kukamilika ujenzi wa ofisi hiyo utagharimu Sh3 bilioni na kwamba kati ya fedha zilizotolewa na Serikali, Sh400 milioni zimetumika kujengea msingi, kauli ambayo ilipingwa na mkuu wa wilaya hiyo, Anna-Rose Nyamubi.


“Waziri Mkuu si kweli kwamba kuna kazi inayoendelea, bali kilichopo pale ni mashimo ambayo hayajulikani ni ya nini. Pia, kuna jengo moja lilijengwa kwa mabati kama stoo hakuna mafundi wanaoendelea na kazi,” alisema Nyamubi.


Majaliwa alisema Serikali ipo katika mchakato wa kuboresha mazingira ya wafanyakazi, ikiwamo ujenzi wa ofisi za watumishi na kwamba haitamvumilia mtu yeyote atayekwamisha juhudi hizo.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza kaimu katibu tawala wa Mara, Raphael Nyanda kutuma timu ya wakaguzi kufanya ukaguzi maalumu katika ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.


Alisema halmashauri hiyo imekuwa na tabia ya kutumia fedha za miradi ya maendeleo kwa shughuli nyingine.


Alikuwa akizungumza na watumishi na madiwani wa Butiama katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere.


Pia, Waziri Mkuu aliagiza kuchunguzwa kwa Solomon Ngiliule, ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Masanja Sabuni (mweka hazina) na Robert Makendo (ofisa ununuzi).

No comments