Breaking News

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AMUAGIZA MRAJIS KUFANYA UCHUNGUZI SACCOS YA MADIBIRA-MBARALI NDANI YA SIKU 14

Na Mwandishi wetu

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mary Mwanjelwa amemuagiza Mrajis Mkuu wa Maendeleo ya Ushirika nchini kuanza uchunguzi mara moja kwenye SACCOS ya Wakulima wa mpunga Madibila iliyoko Wilayani Mbarali, Mkoani Mbeya ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya Watendaji waliohusika na upotevu wa fedha pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.


Mhe Mwanjelwa alitoa agizo hilo Jana Disemba 4, 2018 wakati akipokea taarifa ya kilimo ya Wilaya ya Mbarali akiwa katika ziara yake ya kikazi Wilayani humo.


Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mhe Reuben Mfune alimueleza Mhe Mwanjelwa kuwa katika SACCOS ya Madibila kumekuwa na hasara kubwa kutokana na matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika.


Hivyo alimuomba Naibu Waziri kuwachukulia hatua za kinidhamu haraka viongozi wote waliosababisha hasara kwenye vyama hivyo vya ushirika baada ya uchunguzi kufanyika katika kipindi cha siku 14.


Aliongeza kuwa taarifa ya ukaguzi iliwasilishwa kwa Mrajis wa vyama vya ushirika kwa barua Kumb Na. MDC/C.20/10/89 tarehe 23/01/2017 lakini mpaka sasa hazijachukuliwa hatua zozote za kinidhamu jambo ambalo linafifihisha shughuli za wananchi kujipatia maendeleo endelevu.


Naibu Waziri Mhe Mwanjelwa ametoa wiki mbili (siku 14) kwa Mrajis kufika katika SACCOS hiyo ya Madibira na kutoa majibu haraka ya matokeo ya uchunguzi huo katika kipindi tajwa.


Mhe Mwanjelwa alisema kuwa sekta ya ushirika ni moja kati ya sekta muhimu katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, Vikundi, Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla katika kukuza pato la mwananchi na kupunguza umasikini hivyo ni lazima kuwa na majibu ya haraka pindi kunapobainika uhujumu wa vyama hivyo.


Alisema kuwa Viongozi wa Wilaya zote nchini wana jukumu muhimu la kuhamasisha na kuhiza wanachama kuongeza thamani ya mitaji yao ili kuviwezesha vyama kukuza mitaji ya ndani badala ya kuwa tegemezi kwenye Taasisi zingine za kifedha.


Aidha, Kuendelea kutoa elimu juu ya mfumo wa stakabadhi ya Mazao ghalani ili mkulima apate bei stahiki ya Mazao yake.


No comments