Breaking News

KINONDONI MWENDO WA MAPINGAMIZI...WAGOMBEA WA CHADEMA,CCM NA CUF WATAKIWA KUJIELEZA

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Latifa Almas amesema wagombea watatu katika uchaguzi huo wamewekewa pingamizi.

Akizungumza na Mwananchi jana Januari 22, 2018, Latifa amegoma kuweka wazi aina ya mapingamizi akitaka watafutwe wahusika

Amewataja waliowekewa pingamizi kuwa ni Maulid Mtulia (CCM), Salum Mwalimu (Chadema) na Johnson Mwangosi (Sau).

Amesema watatu hao tayari wameshachukua barua zao za utetezi na kujieleza kuhusu mapingamizi hayo na kutakiwa kuzirejesha haraka iwezekanavyo.

Amesema pingamizi la kwanza ni lile la Mwalimu alilomuwekea Mtulia, la pili ni la Mtulia kumwekea Mwangosi na la mwisho ni la mgombea wa CUF, Rajabu Salum Juma kumuwekea Mwalimu.

"Wagombea wote wameshapata taarifa na tayari wameshachukua barua (fomu) zao za kujieleza wanazotakiwa kuzijaza na kuzirejesha haraka iwezekanavyo. Kama walioweka mapingamizi wasiporidhika na maelezo yao wanaweza kukata rufaa NEC (Tume ya Uchaguzi),” amesema Latifa.

Amesema pingamizi la mwenyekiti wa chama cha Democratic (DP) Mkoa wa Dar es Salaam, David Berege dhidi ya mgombea wa chama hicho, Mary Mpangala limetupiliwa mbali.


"Berege alimpinga mgombea wake wa nafasi wa ubunge jambo ambalo ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na mamlaka husika na tumelitupilia mbali baada ya kulipitia," amesema Latifa.

Chanzo- Mwananchi

No comments