ATCL YADAIWA KUENDELEA KUJIENDESHA KWA HASARA
Kuanzia mwaka 2014/15 hadi 2016/17 matumizi yaliongezeka kwa kiwango cha juu
Dodoma. Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), imetaja mashirika matatu yanayojiendesha kihasara ikiwa ni pamoja na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ambayo imejiendesha kwa hasara kwa miaka mitatu mfululizo.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli zake katika mwaka wa 2017, mwenyekiti wa kamati hiyo, Albert Ntabaliba alisema kamati yake imebaini kuwa taasisi nyingi zimekuwa zikijiendesha kwa hasara kwa sababu mbalimbali ikiwamo matumizi makubwa kuliko mapato.
Alitoa mfano wa ATCL ambayo matumizi yake yamekuwa yakiongezeka kwa kiasi kikubwa na hivyo kuifanya kampuni kujiendesha kwa hasara.
“Katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2014/15 hadi 2016/17 matumizi yaliongezeka kwa kiwango cha juu ikilinganishwa na mapato yaliyokusanywa na kusababisha kampuni kupata hasara kwa miaka yote mitatu mfululizo,” alisema.
Alifafanua kuwa katika mwaka 2014/15 hasara ilikuwa Sh94.3 bilioni, mwaka 2015/16 ilipata hasara ya Sh109.3 bilioni na mwaka 2016/17 ilipata Sh113.8 bilioni na kwamba hali hairidhishi na kama itaendelea kama ilivyo uhai wa kampuni hiyo upo shakani.
Pia, alisema kamati imebaini uwapo wa matumizi makubwa katika Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kuliko mapato, hali iliyosababisha kuwapo kwa nakisi ya Sh397.9 milioni kwa mwaka 2013/14.
Alisema nakisi ya mamlaka hiyo kwa mwaka 2014/15 ilikuwa ni Sh614.6 milioni na mwaka 2015/16, Sh838.2milioni.
“Uchambuzi umebaini kuwa ongezeko hilo kubwa la matumizi limechangiwa na ongezeko la matumizi mengineyo, mishahara na gharama za utawala,”alisema.
Hata hivyo, alisema gharama za uwekezaji (gharama za maonyesho na kutangaza bidhaa na utafiti) zimepungua kutoka asilimia 32.5 mwaka 2011/12 hadi asilimia 16.8 mwaka 2015/16 ambazo zilipaswa kupanda kwa lengo la kukuza kipato cha taasisi hii.
Ntabaliba alisema kamati yake imebaini kuwa Shirika la Elimu Kibaha limekuwa likipata nakisi kwa miaka mitatu mfululizo ya wastani wa Sh1.2 bilioni kwa mwaka.
Alisema mwaka 2012/13, nakisi imeongezeka kutoka Sh482 milioni hadi Sh3.2 bilioni mwaka 2014/15 na kwamba katika miaka miwili ya mwisho, naksi imekuwa ikipungua hadi kufikia Sh955 milioni mwaka 2016/17.
Akichangia taarifa za kamati, Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka alihoji kuwa utafiti gani uliofanyika kabla ya kununua ndege mpya wakati ATCL imeendelea kupata hasara kwa miaka mitatu mfululizo.
“Hali si nzuri kwa kampuni hiyo lakini Serikali imeendelea kununua ndege mpya. Wakurugenzi na bodi inaonyesha wameshindwa kufanya kazi na Serikali isipochukua hatua kampuni hii inakwenda kufa,” alisema.
Vibali vya sukari
Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, imeishauri Serikali iandae utaratibu rafiki wa uingizaji na utoaji sukari ya viwandani bandarini na kurejesha kwa wakati asilimia 15 ya kodi ya sukari ya viwandani.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Suleimain Sadick alishauri wafanyabiashara wawe waaminifu kwa Serikali katika kutoa taarifa za uzalishaji na kodi.
Kamati ya Bunge ya Bajeti imeishauri Serikali kuhakikisha kuwa ukopaji na ulipaji wa deni la Taifa hauathiri ugharamiaji wa bajeti ya Serikali kwa kila mwaka wa fedha.
Akisoma utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo, mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Ghasia aliitaka Serikali kukamilisha kazi ya tathmini ya nchi kukopa na kulipa madeni.
“Aidha Serikali iendelee kufanya majadiliano na taasisi, nchi na Benki ya Dunia wanaoidai nchi ili kupata masharti nafuu katika ulipaji wa Deni la Taifa kama walivyofanya Kenya na Malawi,” alisema.
Ghasia alisema kwa mujibu wa Serikali, deni la Taifa ni himilivu na kwamba fedha nyingi zinazokopwa ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Serikali haijakamilisha tathimini ya uwezo wa nchi kukopa na kulipa madeni ili kuongeza uwezo zaidi wa Serikali kukopa kwenye vyanzo nafuu,” alisema.
Kuhusu sekta ya mabenki, Ghasia alisema hivi karibuni benki zimekumbwa na msukosuko hasa baada ya benki tatu kuwekwa chini ya uangalizi na tano kufungiwa kati ya 15.
Alisema kwa sababu moja ya tatizo kubwa lililozikumba benki hizo ni usimamizi mbovu wa bodi za mabenki hayo, kamati hiyo inaishauri Serikali kupitia Benki Kuu kuanzisha kitengo maalumu chini ya idara ya usimamizi wa mabenki.
Chanzo:Mwananchi
No comments