Breaking News

TANI 400 ZA VIPODOZI HARAMU VYATEKETEZWA TANZANIA

Serikali imesema jumla ya tani 407.82 za vipodozi vilivyopigwa marufuku vyenye thamani ya Sh bilioni 1.36 ziiliteketezwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na kesi 52 zimefunguliwa baada ya upelelezi kukamilika.


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile amebainisha hilo wakati akijibu swali la Mbunge wa Shaurimoyo, Mattar Ali Salum aliyetaka kujua mipango ya serikali katika kudhbiti vipodozi visivyo na viwango pamoja na gharama serikali inazoingia katika udhibiti wa bidhaa hizo.


Amelieleza Bunge, mjini Dodoma leo, Alhamisi, kuwa katika mwaka wa fedha 2016/2017, TFDA ilitenga na kutumia Sh milioni 154.8 kwa ajili ya operesheni ya bidhaa vikiwemo vipodozi. Kwa mujibu wa Naibu Wazir huyo, katika mwaka huu wa fedha , 2017/2018, mamlaka hiyo imetenga Sh milioni 132.2 ambazo zimekuwa zikitumika katika operesheni za kubaini na kukamata vipodozi haramu.


“Katka kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017, maeneo 3,648 yalikaguliwa ambapo kati ya hayo maeneo 120 yalikutwa na vipodozi ambavyo havina viwango na visivyofaa kwa matumizi ya binadamu na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema.


Amesema kwa mujibu wa kifungu cha 91 (b) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, sura 219, kinatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miezi mitatu au kulipa faini ya Sh 500,000 au adhabu zote kwa pamoja kwa yeyote atakayekamatwa akiingiza nchini vipodozi visivyofaa kwa matumizi ya binadamu.

No comments