Watoto 6 Wapandikizwa Vifaa vya Usikivu Muhimbili
Baadhi ya watoto waliofanyiwa upasuaji wa kupandikiza kifaa cha usikivu jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakicheza karata leo. Watoto hao wanaendelea vizuri na matibabu baada ya upasuaji huo.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Pua na Masikio na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Pua na Masikio wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt Edwin Liyombo akipandikiza kifaa cha usikivu kwa mtoto Raiyyan Mshana mwenye tatizo la usikivu baada ya kumfanyia upasuaji leo. Kulia ni Profesa Hassan Wahba kutoka Chuo Kikuu cha Tiba nchini Misri.
Picha ikionyesha jinsi Dkt. Edwin Liyombo akipandikiza kifaa cha usikivu kwa mtoto Raiyyan Mshana mwenye tatizo la usikivu.
Dkt Liyombo akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu watoto waliopandikizwa vifaa vya usikivu baada ya kufanyiwa upasuaji wa masikio.
Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili
………………
Watoto sita wenye tatizo la kutosikia wamefanyiwa upasuaji na kupandikizwa vifaa vya usikivu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Upasuaji huo umeanza Januari 29, mwaka huu na umehusisha wataalam wa Muhimbili kwa kushirikiana na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Tiba Cairo, Misri.
Daktari Bingwa wa Masikio, Pua na Koo Dkt. Edwin Liyombo amesema hii ni ni mara ya pili kwa upasuaji huo kufanyika Muhimbili, upasuaji wa kwanza ulifanyika Juni mwaka jana ambapo watoto watano waliwekewa vifaa hivyo.
Akisisitiza amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili inaendelea kutekeleza azma ya serikali ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi ambao mara nyingi walikuwa wakifuata matibabu yasiyopatikana hapa nchini ama kutokana na kutokuwepo kwa wataalam au ukosefu wa vifaa vya kutolea huduma husika.
“Takwimu za MNH zinaonyesha kuwa asilimia 95 ya wagonjwa ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa kuwekewa kifaa cha usikivu ni watoto wadogo , hivyo huduma hii itasaidia watoto wengi hapa nchini lakini pia inazidi kuwajengea uwezo wataalam wetu wa ndani’’ amesema Dkt. Liyombo.
Kwa mujibu wa Dkt. Liyombo, kupeleka mtoto mmoja nje ya nchi kwa ajili ya kupandikizwa kifaa cha usikivu ni kati ya Shilingi milioni 85 hadi Shilingi milioni 100 wakati gharama ya upasuaji kwa mtoto mmoja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni shilingi milioni 33.
Akielezea ukubwa wa tatizo la kutosikia amesema kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa, watoto watano wanazaliwa na tatizo la kutosikia hivyo kutokana na hali hiyo wazazi wanapaswa kujenga tabia ya kuwapeleka watoto wao hospitalini ili kubaini tatizo mapema.
Katika Hospitali za Umma, Tanzania ni nchi ya kwanza kutoa huduma ya upandikizaji wa vifaa vya usikivu na ya pili kutoa huduma hiyo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki ikitanguliwa na Kenya.
No comments