Breaking News

Wakuu wa Wilaya Mkoani Tabora Watakiwa Kusimamia Sheria Katika Kupamabana na Uharibifu wa Mazingira.

Mkuu-wa-Wilaya-ya-Tabora-Queen-Mlozi-660x330
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora Queen Mlozi.

NA TIGANYA VINCENT RS TABORA
Wakuu wote wa Wilaya na Watendaji wa ngazi mbalimbali kuhakikisha wanatumia Sheria mbalimbali zikiwemo ndogo ndogo katika kupambana watu wote wanaoendesha vitendo vya uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji ovyo wa mistu.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora Queen Mlozi wakati wa uzinduzi wa wiki ya upandaji wa miti kwa kutumia Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NGO’s)ambayo yanafanya kazi mkoani humo.
Alisema kuna sehemu watu wamekuwa wakiendesha uharibifu wa mazingira na mistu kwa sababu ya baadhi ya watendaji kushindwa kusimama katika nafasi zao za kutumia Sheria zilizopo kuzuia uharibifu ambao ukiendelea kama vile kulisha mifugo miti inayopandwa, kuchoma moto miti na kukata ovyo miti kwa ajili ya mkaa na shughuli nyingine za kibinadamu.
Queen alisema juhudi zinazoendelea kuugeuza Mkoa wa Tabora kuwa wa kijani zitakwama kama watendaji mbalimbali katika nafasi zao watashindwa kusimamia Sheria ili kuhakikisha hakuna uharibifu unaofanyika katika mistu asili na hata ile ya kupandwa.
Katika hatua nyingine Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora aliwaagiza Wakuu wote wa Wilaya na Watendaji mbalimbali kuhakikisha Mashirika yote yasiyokuwa ya Kiserikali (NGO’s) ambayo yanaendelesha shughuli zake mkoani yanashiriki kikamilifu katika upandaji miti na uhifadhi wa mazingira katika kipindi cha wiki hii.
Alisema kila mdau anayeishi Mkoani Tabora ni lazima ashiriki katika kampeni ya upandaji miti kwa kuwa zoezi hilo sio la kundi fulani bali ni la wadau wote bila kujali itikadi, dini zao na kazi zao.
Kwa upande wa Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Hajjat Rukia Manduta alisema kuanza sasa hawatasaji Shirika jipya lisilokuwa la Kiserikali (NGO) ambalo katika mipango yake halitatoa kipaumbelea katika mipango yake suala la upandaji miti na utunzaji wa mazingira.
Alisema kabla ya kupata usajili ni vema katika shughuli zao wanazotaka kuzifanywa waonyeshe pia jinsi watakavyoshiriki katika  zoezi la kuhakikisha mazingira yanakuwa endelevu na upandaji miti.
Hajjat Rukia  alisema lengo ni kutaka kuzifanya NGOs zote Mkoani Tabora kuwa ni sehemu ya mpango wa kuufanya Mkoa wa Tabora wa kijani katika kipindi cha miaka michache ijayo.
Naye Afisa Habari wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Jikombee Integral Development Association (JIDA) John Pinini alisema alisema wamelipokea zoezi hilo hilo kwa furaha kubwa kuwa wanatambua kuwa ili waendelee kutekeleza majukumu yao ni lazima watu wawepo.
Alisema kuwa bila mazingira kuwa endelevu watu wanaweza wasiwepo na hivyo kuwa ndio mwisho wa shughuli zao
Pinini aliongeza kuwa watambua miti ndio uhai na bila miti hakuna uhai na hivyo wadau wanaofanya nao kazi hawatakuwepo na hivyo hakutakuwepo wa kuwahudumia kama mazingira yatakuwa yameharibika.
Wiki ya upandaji miti kwa kutumia NGO imeanza juzi na itamalizika siku ya Jumamosi ambapo Mashirika kama vile Jikombee Integral Development Association (JIDA) ,Spiritual Life in Christ(SLIC) na Tupambane na UKIMWI Tanzania(TUKUTA) yameshiriki katika uzinduzi wa zoezi hilo wilayani Uyui

No comments