AGAPE NA POLISI WATOA ELIMU JUU YA MADHARA YA MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI KWA WANAFUNZI WA SHULE ZA KATA YA DIDIA SHINYANGA
Shirika lisilo la kiserikali la Agape AIDS Control Programme (AACP) kwa kushirikiana na jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga kupitia dawati la jinsia na watoto wametoa elimu kuhusu madhara ya ndoa na mimba za utotoni na jinsi ya kutoa taarifa za matukio ya ukatili dhidi ya watoto kwa wanafunzi wa shule sita zilizopo katika kata ya Didia Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Elimu hiyo imetolewa leo Alhamis Februari 1,2018 kwa wanafunzi wanaosoma katika shule ya msingi Didia, Bukumbi,Bugisi,Mwanono,Mwamalulu na shule ya sekondari Didia.
Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda alisema elimu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa na shirika la AGAPE kwa ufadhili wa shirika la kimataifa la Firelight Foundation.
“Tunawaelimisha wanafunzi kuhusu madhara ya mimba na ndoa za utotoni na jinsi ya kutoa taarifa juu ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto kwa lengo la kuongeza nguvu kutokomeza mimba za wanafunzi shuleni na ndoa za utotoni na matukio mengine ya ukatili”,alieleza Isabuda.
“Kupitia elimu hii tunawajengea uwezo wanafunzi hawa ili waweze kupaza sauti juu ya matukio ya kikatili na watoe taarifa za matukio hayo katika ngazi mbalimbali”,aliongeza.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE, John Myola aliwataka wanafunzi kuzingatia masomo shuleni na kuhakikisha wanaepuka vishawishi mbalimbali wanavyokutana navyo ikiwemo kurubuniwa kwa chips,kupewa lifti na waendesha bodaboda na kupokea zawadi kutoka kwa watu wasiowafahamu pia kujihusisha mahusiano ya kimapenzi kwani matokeo yake ni kupata mimba ama kuambukizwa magonjwa ya zinaa.
“Hatutaki kusikia watoto wanakatisha masomo kwa sababu ya mimba ama ndoa za utotoni,tutaendelea kushirikiana na jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia kupigania watoto”,aliongeza Myola.
Naye Secilia Kizza kutoka dawati la jinsia na watoto jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga aliwasihi wanafunzi hao kutoa taarifa za matukio ya ukatili dhidi ya watoto ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Nao wanafunzi kutoka shule hizo walilishukuru shirika la AGAPE kwa kuwafikia na kuwapa elimu hiyo ambapo waliahidi kuendelea kupeana elimu wao kwa wao kupitia “Klabu za Tuseme” zilizoundwa na shirika hilo katika kila shule.
Shirika la AGAPE linaendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya mimba na ndoa za utotoni katika shule 13 za wilaya ya Shinyanga kati ya hizo sita zipo katika kata ya Didia.
Shule zingine ni shule za msingi Ndala A,Ndala B,Bushola,Ujamaa,Twende pamoja,Mwamalili na shule ya sekondari Masekelo zilizopo katika halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda akitoa kuhusu madhara ya ndoa na mimba za utotoni kwa wanafunzi wa shule ya msingi Didia iliyopo katika kijiji cha Didia kata ya Didia halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (Vijijini). Kulia ni Secilia Kizza kutoka dawati la jinsia na watoto jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga.
Wanafunzi wa shule ya Msingi Didia wakimsikiliza Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda.
Isabuda akiendelea kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule ya msingi Didia.
Secilia Kizza kutoka dawati la jinsia na watoto jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga akitoa elimu kuhusu madhara ya ndoa na mimba za utotoni kwa wanafunzi wa shule ya msingi Didia.
Kulia ni mwanafunzi wa shule ya msingi Bukumbi iliyopo katika kijiji cha Bukumbi kata ya Didia akielezea namna wanavyofundishana kwenye "Klabu za Tuseme" kuhusu haki za watoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE, John Myola akiwaasa wanafunzi wa shule ya msingi Bukumbi kuepuka vishawishi ili waweze kumaliza masomo yao vizuri na kutimiza ndoto zao.
Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda akiuliza wanafunzi wangapi katika shule ya msingi Bukumbi wapo tayari kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Secilia Kizza kutoka dawati la jinsia na watoto jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga akiwapa wanafunzi mbinu za kutoa taarifa wanapoona matukio ya kikatili.
Kulia ni mwanafunzi wa shule ya msingi Bukumbi akiuliza swali kwa maafisa wa shirika la AGAPE.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bukumbi, Tumaini Ngusulu akiwashukuru maafisa kutoka AGAPE kwa kutoa elimu juu ya madhara ya mimba na ndoa za utotoni.
Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE, John Myola na Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda wakijitambulisha kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Didia iliyopo katika kata ya Didia.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE, John Myola akiwataka wanafunzi wa shule ya sekondari kuacha kujihusisha na mapenzi wao kwa wao ama na watu wengine bali wazingatie elimu kwani ndiyo urithi wa kudumu katika maisha yao.
Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda akiwasisita wanafunzi wa shule ya sekondari Didia kuzingatia masomo yao na kuwa walinzi kwa wenzao ili kuhakikisha kila mwanafunzi anamaliza masomo yake vizuri.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Didia wakifuatilia somo.
Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda akiwaasa wanafunzi kuhudhuria masomo darasani na kutoa taarifa wanapoona vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
No comments