Breaking News

SIMIYU YAPATIWA CHUPA MIL 2 ZA KUUA WADUDU WA PAMBA

Dawa za kuua wadudu wa pamba
Dawa za kuua wadudu wa pamba

 Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akipata maelezo namna wadudu wanavyoshambulia zao la pamba kutoka kwa mkaguzi wa pamba wilaya ya Bariadi Alfred Chagula, walipotembelea mashamba ya wakulima jana Mbiti.

Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Mathew Mtigumwe (mwenye miwani) akimsikiliza mkulima wa pamba Tindigwe Masuke wa kijiji cha Mbiti alipokuwa akiongelea juu ya uhaba wa dawa, unaowakabili wakulima hao.

Serikali imewahakikishia wakulima wa pamba Mkoani Simiyu kuwapatia pembejeo za kilimo ili kukabiliana na wadudu waharibifu ambao wameanza kushambulia zao hilo.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe alipofanya ziara ya kukagua mashamba ya wakulima na kujionea changamoto zinazowakabili, ikiwemo mazao yao kushambuliwa na wadudu katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.

"Tumeanza kusambaza pembejeo kwa wakulima mkoani Simiyu baada ya kuona mahitaji ya dawa ni makubwa…awali tulipanga kusambaza chupa milioni 1.8, Lakini mahitaji yamekuwa ni makubwa tumeongeza na kufikia chupa milioni 2 ili kusuru zao hilo",alisisitiza Katibu mkuu.

Aliongeza kuwa wizara ya kilimo imesambaza watalamu 30 nchini ili kusaidiana na wataalamu kilimo ngazi ya mkoa, wilaya na kata katika kutoa elimu kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya dawa, pia namna ya kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao.

Mtigumwe aliwataka wataalamu wa kilimo kutoa elimu kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo ili kuhakikisha dawa zinazosambazwa zinatumika ipasavyo.

Tindigwe Masuke mkulima wa Pamba kijiji cha Mbiti alisema kuwa dawa zinazosambazwa na serikali hazitoshelezi mahitaji ya wakulima ambao wahamasika kulima, wamekuwa wakipata kidogokidogo hali inayowafanya kushindwa kuwakabili wadudu wa pamba.

Kwa upande wake Meneja wa Bodi ya pamba kanda ya Ziwa, Jones Bwahama alisema kuwa serikali kwa kusirikiana na bodi ya Pamba imeleta timu ya wataalamu saba katika mkoa wa simiyu ili kusaidia na maafisa ugani kuelimisha wakulima jinsi ya matumizi sahihi ya pembejeo.

Mkoa wa Simiyu unahitaji chupa za dawa 1,810,839 huku kukiwa na jumla ya wakulima wa pamba 309,511 ambao wamelima ekari 602,409 likitarajiwa kuzalisha tani 421,686.3 za pamba kwa wastani wa kilo 700 kwa ekari moja.

Na Costantine Mathias - Simiyu 

No comments