MSUKUMA AMCHANA WAZIRI WA JPM...AMTAKA ASIFANYE KAZI KWA MIHEMUKO
Mbunge na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma amemshambulia kwa maneno Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina juu ya 'operation' anazozifanya za kionevu za kupambana na uvuvi haramu kwa kumwambia aache kufanya kazi kwa mihemuko.
Msukuma ameeleza hayo katika mkutano wa 10 kikao cha sita cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma wakati akichangia uwasilishaji wa kamati ya kudumu ya Bunge ya kilimo, mifugo na maji baada ya kupita miezi kadhaa tokea Waziri Mpina kutoa kauli yake kuachia madaraka endapo tatizo la uvuvi haramu litaendelea kuwa sugu nchini jambo ambalo kwa sasa Msukuma anadai kiongozi huyo analifanya bila ya kufuata sheria zilizopo kwa kuzuia watu wasivue dagaa na kupelekea kuwapa athari wananchi wanyonge na kumuomba aundiwe tume ya uchunguzi yeye timu yake.
"Toka nazaliwa sijawahi kuona sheria hizi zinazotumiwa na Waziri wa Mifugo Mpina, umri wangu huu nimeshuhudia awamu zote za Mawaziri. Nafikilia kwamba ndio tunaanza kutunga sheria au hii ilikuwa imefichwa ndio inaibuka. Sijawahi kuona Waziri anasimama na kujisifu kwamba kwao hakuna samaki na kutamani watu wote wasile samaki. Mungu ametupa neema tofauti, sijawahi kuona mtu anaenda kukamata mitego dakika mbili faini hana unachoma nyavu zake bila ya kuhakikisha kwamba ni feki au laa",amesema Msukuma.
Aidha, Msukuma amesema ana muhitaji Waziri huyo siku akihudhuria Bunge basi aweke wazi kuhusiana na sheria hizo anazozitumia amezitoa wapi na kama akishindwa kutokea katika kipindi basi watamsubiri katika Bunge la bajeti ili wambane vizuri juu ya hilo.
"Nitoe rai kwa Mawaziri kwamba Mawaziri wa aina kama hii nina washauri wapunguze mihemuko kwa sababu hata sisi tunatamani kuendelea kuwa Wabunge humu ndani lakini kwa 'dizaini' mnayoenda mtuambie mmewapanga wabunge wa kina nani ambao mnataka wawe wabunge maeneo yetu. Nina zungumza kwa wabunge wanaotoka Kanda ya Ziwa sidhani kama sisi tutarudi humu Bungeni", amesisitiza Msukuma.
Kwa upande mwingine, Msukuma amemtaka Waziri Mpina na timu yake kiujumla wajipange kuwafundisha wavuvi na wala sio kuwafilisi.
No comments