Serikali Mkoani Geita imeeleza kusikitishwa na uendeshwaji wa miradi ya mgodi wa dhahabu wa Geita, (GGM) kwa kutozingatia sheria ya ushirikishaji kwa Halmashauri zilizopo mkoani humo na kushindwa kujulikana kwa gharama za miradi ya jamii inayotekelezwa na mgodi huo.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kukabidhi mradi wa Maendeleo ya uchumi kwa Vijana na Wanawake ulipo Mtaa wa Magogo Kata ya Bombambili Halmashauri ya Mji wa Geita.
Hali hiyo ilimlazimu Mkuu wa mkoa wa Geita ,Mhandisi Robert Luhumbi kuzulu kwenye mradi wa vijana na wanawake uliopo kata ya Bomba mbili ,mtaa wa magogo kwa lengo la kujiridhisha baadhi ya vifaa ambavyo vilitakiwa kuwepo kwenye mradi huo na hata hivyo amebaini kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kwenye vifaa ambavyo vilitakiwa kuwepo kwenye mradi huo.
Luhumbi alisema baadhi ya watumishi kutoka serikalini na baadhi yao kutoka GGM wameendelea kushirikiana kwa pamoja kuhujumu miradi mingi ambayo imekuwa ikilenga kuleta chachu ya maendeleo kwa wakazi wa Geita ambao wamezungukwa na Mgodi huo na kufuatia hatua hiyo ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike ili kuwabaini wale wote ambao wameshiriki kuchakachua fedha za miradi hiyo.
“Sasa katika miradi yote ishirini na sita (26) ambayo imekwenda yote ina matatizo na ajabu mwaka huu niliambiwa kuna fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya CSR ya mwaka huu nilikagua baadhi ya miradi kuna mradi mmoja nilikuta ni wa bilioni moja nukta sita lakini mimi siwezi kuficha hata tukitumia fedha vibaya kidogo tunaweza kutumia milioni mia tatu (300) lakini bilioni moja nukta tatu inapotea na watu kutoka ofisi zetu walikwenda mgodini wakaa na kuweka mkataba wakurugenzi hawakuwepo mkuu wa wilaya afahamu baadae tunaambiwa fedha ipo tayari kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo nimesema sisi kama mkoa hatubariki miradi hiyo kabisa”Alisema Luhumbi.
Hata hivyo kutokana na kuonekana upungufu kwenye miradi ya jamii Mhandisi Luhumbi amewakataa maafisa mahusiano ya jamii wa mgodi wa GGM kutokana na kushindwa kufanya shughuli zao kwa weledi kwenye maeneo waliyopangiwa na mgodi huo.
Na pia ameviagiza vyombo vyote vya sheria kuhakikisha wanaingia kwa undani zaidi na kufanya uchunguzi wa kutosha na ndani ya wiki moja endapo kuna mtumishi wa serikali atakayebainika kuhujumu basi sheria ichukuliwe dhidi yake ikiwa ni pamoja na kumwajibisha.
Afisa sheria wa Mkoa huo Bi Sarah Mwangole alisema mradi wa Magogo ambao umekabidhiwa hivi karibuni umefanyika bila ya makubaliano baina ya Halmashauri na mgodi wa GGM hivyo pia wameshauri vyombo vya sheria kuingilia na kufanya uchunguzi na kwamba hadi sasa ofisini kwao hawajapata nyaraka zozote za mradi huo licha ya kuzihitaji.
Mtandao huu umezungumza na Msimamizi wa kitengo cha mahusiano kwenye mgodi wa GGM Bw Joseph Mangilima ambaye alisema mengi ya mambo yaliyozungumziwa hawezi kuyazungumzia yeye kwa kuwa hayahusiani na kitengo chake moja kwa moja na kwamba kazi iliyompeleka kwenye mradi huo ni kupeleka funguo za majengo baada ya kusikia mkuu wa mkoa anautembelea mradi huo.
No comments