WAZAZI WAASWA KUWASOMESHA WATOTO WA KIKE
WAZAZI na Walezi wameaswa kuwasomesha watoto wa kike na kuachana na
fikra potofu kuwa kumsomesha mtoto wa kike ni kupoteza rasilimali fedha kwani
maisha ya sasa bila elimu ni changamoto kubwa kwa mtoto wa kike.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Kenneth Komba kutoka Idara ya
Elimu mkoa wa Iringa kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza wakati
alipokuwa mgeni rasmi wakati wa mahafali ya kumi kidato cha nne katika shule ya
Sekondari ya Wasichana ya Spring Valley iliyopo Mkoani Iringa.
Alisema kuwa mtoto wa kike akipatiwa elimu kuna uwezekano mkubwa kwa
taifa kuwa na maendeleo kutokana na kuwajibika kwao katika maisha ya kila siku
hivyo wazazi na walezi ni muhimu kuwasomesha watoto wa kike kwa lengo la kuendeleza
ndoto walizonazo.
Alisema kuwa jukumu la kusomesha elimu ya msingi hadi sekondari ni la
serikali lakini wazazi na walezi wanaosomesha shuleni hapo ni kuisaidia
serikali hivyo ipo tayari kupokea changomoto zote katika shule hiyo na
kushirikiana kuzitatua.
Komba aliipongeza shule ya sekondari Spring Valley kwa kuwa moja ya
shule zinazofanya vizuri mkoani hapa kielimu na tabia kwani ni moja ya shule
ambazo idara ya elimu haipati malalamiko ya mara kwa mara kutoka shuleni hapo.
Aidha Komba aliwataka wahitimu hao kusoma mazingira ya maisha popote
watakapokuwa na kuamua namna ya kujiajiri ili mradi isiwe shughuli
zinazopingana na sheria na maadili ya kijamii, kama vile kuuza madawa ya
kulevya, ukahaba, unyang'anyi na mambo mengine yanayofanana na hayo ambayo
watajiingiza matatani na kuonekana wabaya.
Awali mkuu wa shule ya Wasichana Spring Valley, Adia Mbwanji alisema
kuwa uongozi wa shule hiyo umeweka mikakati mbalimbali itakayotekelezwa mwaka
2018 ikiwemo ujenzi wa ukuta upande wa Kusini mwa shule, upanuzi wa maktaba,
ununuzi wa gari la shule na kukarabati mifumo ya maji taka na maji safi.
Alisema kuwa shule hiyo inayomilikiwa na kanisa la Baptist Convention
of Tanzania imejipanga kujenga chumba cha kompyuta na kununua komputa zenyewe
ili kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi kuendana na ulimwengu wa sayansi na
teknolojia.
Kwa upande wao wahitimu kwa kupitia msoma risala, Happy Njavike
walisema kuwa shule hiyo inatakiwa kuboresha ujenzi wa jengo la maabara vifaa
vyake vinunuliwe ili kutoa fursa kwa wanafunzi wengi kujifunza kwa vitendo hasa
masomo ya sayansi kwa lengo la kukuza ufaulu na kuongeza ujuzi katika masomo ya
sayansi.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya
wasichana ya Spring Valley iliyoko katika manispaa ya Iringa wakiwa katika
mafunzo ya vitendo shuleni hapo.
wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana
ya Springa Valley wakiwa katika picha ya pamoja.
No comments