Lulu Michael Ahukumiwa Kifungo cha Miaka Miwili Jela
Msanii wa Filamu Elizabeth Michael Lulu akiingia katika Mahakama Kuu Dar es Salaam leo kabla ya kusomewa hukumu yake.
Mama wa Msanii wa Filamu Elizabeth Michael Lulu, Lucresia Karugila
akitoka katika chuma cha Mahakama Kuu Dar es Salaam, kwa huzuni baada ya
mwanae kuukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.
Na Mwandishi wetu
Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imemhukumu
kwenda jela miaka miwili muigizaji wa filamu bongo Elizabeth Michael (Lulu)
ambaye alikuwa anakabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Jaji Sam Rumanyika aliyekuwa
anaendesha kesi hiyo, na kusema kwamba mshtakiwa amekutwa na hatia ya kuua bila
kukusudia kutokana na ushahidi wa mazingira, hivyo atatumikia kifungo cha miaka
miwili jela.
"Ushahidi wa mazingira unaweza kutumika kama msingi pekee
wa kumtia hatiani mshtakiwa tena mshtakiwa pekee, sasa ninapokwenda kuangalia
maelezo ya mshtakiwa kama yanakidhi vigezo nilivyosema awali, kwa mujibu wa
mshtakiwa alisema alianza kupigwa na marehemu, marehemu alilewa lakini kuhusu
mshtakiwa anatakiwa kutoa maelezo yanayo jitosheleza, kwa hili mshtakiwa
alijikanganya" amesema Jaji Rumanyika.
Jaji Rumanyika ameendelea kwa kusema kwamba.."mshtakiwa
katika maelezo yake hakueleza kuwa marehemu alianguka au laah wakati
anamkimbiza, maelezo ya Dkt. Josephine siyo maelezo ya cheti cha hospitali,
hayakuwa na hadhi ya hospitali".
"Inakinzana na hekima ya kawaida kwamba hata pale marehemu
alipoendelea kumpiga na kumshambulia na akaenda kiwango cha kumtishia kumuua,
mstakiwa hakuthubutu hata kumpiga, ina maana alifanya kama maneno ya biblia
yanavyosema mtu akikupiga shavu la kushoto mgeuzie na la kulia lakini hili
mshtakiwa hakulisema.", amesema Jaji Rumanyika.
"Na wakati huo mshtakiwa alikuwa na miaka 17, leo ana miaka
22, alikuwa mtoto hivyo asingetambua kuwa kinachofanyika ni kibaya au kizuri,
huyu mtoto sio mshtakiwa aliyelengwa nasheria ya watoto, kama mtoto wa umri huu
na anaweza kafanya ya watu wazima, mahakama hii haikubaliani bali
mshtakiwa ni mkomavu, hakuna mashaka kuwa kifo cha marehemu kilitokana na
ugomvi", ameendelea kusema Jaji Rumanyika mahakamani hapo.
Baada ya hapo jaji rumanyika aliwapa nafasi upande wa mshtakiwa
kujitetea ambapo wakili wake Peter Kibatala alimtetea mshakiwa kwa kusema kuwa
mshtakiwa anategemewa na familia yake.
Baada ya hapo Jaji Rumanyika alitoa hukumu yake na kumuamuru
mshtakiwa kwenda jela kwa miaka miwili.
Elizabeth Michael (Lulu) anahukumiwa kwa kumuaa aliyekuwa mpenzi
wake Steven Charles Kanumba ambaye pia ni muigizaji mwenzake, mnamo April 7,
2012.
No comments