Breaking News

SHIRIKA LA SAVE THE CHILDREN LATOA MSAADA WA PIKIPIKI KWA JESHI LA POLISI SHINYANGA

Shirika la kimataifa la Save The Children limetoa msaada wa pikipiki kwa ajili ya dawati la jinsia na watoto la jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.


Akizungumza leo Ijumaa Novemba 10,2017 wakati wa kukabidhi pikipiki moja kwa jeshi la polisi,Meneja wa shirika la Save The Children mkoa wa Shinyanga Benety Malima alisema pikipiki hiyo itasaidia katika ufuatiliaji wa makosa mbalimbali yakiwemo ya jinai.


“Shirika letu limekuwa likiendesha mafunzo kuhusu ukusanyaji wa vielelezo kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi kwa ushahidi mahakamani,tumebaini kuwa miongoni mwa changamoto zilizopo ni usafiri,kutokana na hali hiyo tumeona tuangalie namna ya kuwezesha usafiri ili kukabiliana na vitendo vya ukatili katika jamii”,alieleza Malima.

Akipokea pikipiki hiyo SSP Lutusyo Mwakyusa aliyemwakilisha kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule,alilishukuru shirika hilo kwa kuona umuhimu wa kusaidia jeshi la polisi. 

“Tunalishukuru shirika la Save the Children, huu ni msaada mkubwa sana kwetu kwani utasaidia kuokoa maisha ya watu,na hiki ni kielelezo tosha cha ushirikiano kwa vitendo katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia,naomba wadau wengine waige mfano wa shirika hili ili kujenga jeshi letu la polisi”,alieleza Mwakyusa. 

Aliwataka wadau kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi ili kuhakikisha kuwa matukio ya ukatili yanatokomezwa.

Meneja wa Shirika la Save The Children Mkoa wa Shinyanga Benety Malima akikabidhi funguo ya pikipiki kwa SSP Lutusyo Mwakyusa

Mwakilishi wa kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SSP Lutusyo Mwakyusa akijaribu kuendesha pikipiki iliyotolewa na shirika la Save The Children.


No comments