WAGONJWA 15 WAFANYIWA UPASUAJI WA KUPANDIKIZA MISHIPA YA DAMU KATIKA MOYO NA KUREKEBISHA MSHIPA MKUBWA WA DAMU KATIKA KAMBI MAALUM YA MATIBABU.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee ya Mjini Mumbai nchini India wamefanya
upasuaji mkubwa wa moyo kwa wagonjwa 15 katika kambi maalum ya upasuaji ya siku
sita inayomalizika kesho.
Upasuaji wa moyo
unaofanyika katika kambi hii ambayo imeanza Jumatatu tarehe 8/11/2017 hadi
Jumamosi tarehe 11/11/2017 ni ya upasuaji wa kufungua kifua kwa watu wazima.
Upasuaji uliofanyika ni wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (CABG –
Coronary Artery Bypass Grafting), na kubadili milango miwili hadi mitatu ya
moyo (Valve Replacement).
Kwa mara ya kwanza
hapa nchini tumefanya upasuaji wa kurekebisa mshipa mkubwa unaotoa damu kwenye
moyo kwenda sehemu zote za mwili (Aortic Aneurysm Repair).
Tulifanya upasuaji
kwa wagonjwa watatu kwa siku, wote hawa wanaendelea vizuri na wataruhusiwa
pindi afya zao zitakapoimarika. Baadhi yao ambao tumewafanyia upasuaji jana na
juzi wako katika chumba cha uangalizi maalum na wengine wako wodini wameshaanza
kufanya mazoezi.
Kama wagonjwa hawa
wangeenda kutibiwa nje ya nchi Serikali ingelipia zaidi ya milioni 405 kwani
gharama za mgonjwa mmoja kwenda kutibiwa nje ya nchi ni zaidi ya milioni 27.
Gharama za matibabu haya hapa nchini kwa wagonjwa 15 ni milioni 225 (milioni 15
kwa mgonjwa mmoja).
Changamoto kubwa
tunayokabiliana nayo katika matibabu ya wagonjwa wetu ni wagonjwa wengi
tunaowapokea mioyo yao kutokuwa katika hali nzuri. Tunawashauri wananchi
kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara hii itawasaidia kujuwa kama wana
matatizo ya moyo au la na hivyo kupata tiba kwa wakati.
Kama mnavyofahamu
matibabu ya moyo ni ya gharama hivyo basi tunaendelea kuwahimiza wananchi
kujiunga na mfuko wa taifa wa bima ya afya ambao utawasaidia kulipa gharama za
matibabu pindi watakapougua na kuhitaji kupata matibabu.
Kwa namna ya kipekee
Taasisi inaishukuru Hospitali ya Seifee kutokana na ushirikianao mzuri
tuliokuwa nao, licha ya kutoa matibabu kwa wagonjwa tumekuwa tukibadilishana
ujuzi wa kazi wakati wa kufanya upasuaji. Kwa mwaka huu hii ni mara ya pili kwa
wataalamu hawa kuja katika Taasisi yetu. Mwezi wa tatu mwishoni tulifanya nao
kambi ya upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa nane (8).
Aidha tunatarajia
kuwa na kambi maalum ya matibabu ya moyo ya bila kufungua kifua kwa kutumia
mtambo maalum wa Cathlab kwa watu wazima itakayoanza tarehe 14/11/2017
hadi tarehe 19/11/2017. Katika kambi hii ambayo tutashirikiana na wenzetu
kutoka Taasisi ya Sharjah Charity kutoka Falme za Kiarabu tunatarajia kufanya
upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 50.
Tunawaomba wananchi
waendeleee kuchangia damu kwani wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo
wanahitaji kuongezewa damu wakati wanapatiwa matibabu. Mgonjwa mmoja anahitaji
damu kati ya chupa 5 hadi 6.
Kwa mtu mmoja mmoja
au kikundi cha watu ambao wanapenda kuchangia damu tunawaomba wafike Taasisi ya
Moyo iliyopo Muhimbili mkabala na Maabara kuu. Kwa maelezo zaidi wawasiliane
kwa simu namba 022-2151379 au 0713304149.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo na Mishipa ya Damu ambaye
pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Bashir Nyangasa akiongea na waandishi wa Habari leo jijini Dar
es Salaam kuhusu kambi maalum ya upasuaji ambayo imefanywa na Taasisi hiyo kwa
kushirikiana na Hospitali ya Saifee ya Mjini Mumbai nchini India ambapo
wagonjwa 15 wamefanyiwa upasuaji. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Uuguzi Roberth Mallya na kushoto ni Daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa
mahututi Anjela Muhozya akifuatiwa na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo na
Mishipa ya Damu kutoka Hospitali ya Saifee Ali Ascar Beliranwalwa.
Daktari Bingwa wa Upasuaji
wa Moyo na Mishipa ya Damu ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Bashir Nyangasa akiongea na
waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu kambi maalum ya upasuaji
ambayo imefanywa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee ya
Mjini Mumbai nchini India ambapo wagonjwa 15 wamefanyiwa upasuaji. Kushoto ni
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi Roberth Mallya na kushoto ni Daktari bingwa
wa usingizi na wagonjwa mahututi Anjela Muhozya akifuatiwa na Daktari Bingwa wa
Upasuaji wa Moyo na Mishipa ya Damu kutoka Hospitali ya Saifee Ali Ascar
Beliranwalwa.
No comments