Breaking News

Diaspora yamuunga mkono Rc Makonda ujenzi ofisi 402 za walimu

Jumuiya ya watanzania wanaoishi Diaspora (Marekani) ijulikanayo kama  Sixth Region Diaspora Caucus Washington kwa pamoja wameamua kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh Paul Makonda kutatua changamoto za ofisi za walimu wa mkoa huu kwa kutoa makontena 36 ya samani mbalimbali zikiwemo viti vya kisasa zaidi ya 5000,meza za umeme 2500,meza za kawaida 2500,makabati ya vitabu makubwa 1300 na bao (writing boards) za kuandikia 700

Mchango huu wa samani ambao una thamani ya zaidi ya dola za kimarekani $ 800,000 ambazo ni sawa na shilingi 1,800,000,000 za kitanzania utatumika katika ofisi mpya 402 za walimu zilizoanza kujengwa kupitia kampeni iliyoanzishwa na Mh Paul Makonda mapema Agosti mwaka huu.

Kupitia samani hizi adhma ya Mh Paul Makonda ya kutengeneza mazingira rafiki ya utoaji wa elimu kwa walimu wa Mkoa wa Dar es salaam itakuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana na matarajio ya kupandisha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi kufikiwa kama matokeo ya miundo mbinu rafiki kwa wote.

Makontena hayo yanatarajiwa kufika nchini mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka huu.

Mh Makonda amewashukuru wadau hawa ambao bila kuzingatia umbali waliopo na nchi yao bado wameonyesha hari ya kuguswa na changamoto za watanzania wenzao hapa nchini, na kutoa rai kwa watanzania wengine kuendelea kuunga mkono kampeni hii ya ujenzi wa ofisi 402 za walimu Dar es salaam kwa namna watakavyo weza kwani hatma ya ustawi wa maendeleo ya Tanzania ni wajibu wa kila mtanzania.

Imetolewa na kitengo cha habari na uhusiano,ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar es salaam.

No comments