Benki ya Absa Tanzania yazindua akaunti ya akiba ya kikundi.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Ndabu Swere (katikati), akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi rasmi wa akaunti ya akiba ya kikundi ya benki hiyo jijini Dar es Salaam leo. Wanaoshuhudia ni Meneja wa Huduma za Jamii wa Absa, Bi. Abigail Lukuvi (kushoto) na Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi wa benki hiyo, Heristraton Genesis.
Benki ya Absa Tanzania imezindua bidhaa mpya, Akaunti ya Akiba ya Kikundi, inayolenga kuwawezesha watu wanaokusudia kufikia malengo ya kifedha ya pamoja kuweza kuweka akiba na kuwekeza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kuharakisha ajenda ya ujumuishaji wa kifedha nchini Tanzania.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki hiyo, Bi. Ndabu Swere alisema: “Akaunti ya Akiba ya Kikundi ya Absa inakusudiwa kwa ajili ya vikundi; kupitia akaunti hii, tunaviwezesha vikundi kuweka akiba, kuwekeza, na kupata riba.”
Alibainisha kuwa akaunti hiyo ina faida kadhaa, kubwa ikiwa ni urahisi wake unaowawezesha wamiliki kufanya miamala popote kwa kutumia mifumo ya kidijitali ya benki, benki wakala, au hundi.
Aliongeza: “Akaunti hii pia ni wazi, kwani wamiliki wanapata taarifa kuhusu kinachoendelea kwenye akaunti, kama vile uwekaji na utoaji pesa, wanaweza kuona akaunti na pia kupata taarifa za mara kwa mara.”
Faida nyingine, alibainisha, ni kwamba wamiliki wanapata bima, ambayo inaweza kutoa fidia endapo kutatokea matukio yasiyotabirika kama kifo cha mmiliki wa akaunti au ndugu zao wa karibu.
Akaunti hii pia inajenga hisia kubwa ya uwajibikaji ambayo haiwezekani kwa mtu mmoja mmoja; kama kikundi, wanaweza kuweka akiba na kufanikiwa, kwa sababu kila mwanachama anahisi wajibu wa kufanya kazi kuelekea kufanikisha malengo ya pamoja yaliyokubaliwa.
Faida nyingine ya akaunti hii ni usalama, kwani akaunti itakuwa salama kutokana na ukweli kwamba mifumo ya Absa imeundwa kuhakikisha usalama wa fedha za wateja; majukwaa yetu ni salama kabisa.
“Natoa wito kwa vikundi visivyo na akaunti, vikundi vyenye akaunti lakini ambazo hazina sifa za Akaunti ya Akiba ya Kikundi ya Absa, na watu binafsi wasio na vikundi kufanya maamuzi ya kutumia pendekezo hili lenye thamani,” alisema Bi. Ndabu.
Alibainisha kuwa bidhaa hii mpya ni sehemu ya juhudi za benki hiyo sambammba na lengo kuu la benki hiyo la ‘kuiwezesha Afrika ya kesho pamoja – hatua moja baada ya nyingine’ kusaidia bara hili kushinda changamoto zake za kijamii na kiuchumi.
“Iwapo wateja wetu watafanikiwa kufikia malengo yao ya pamoja kupitia Akaunti ya Akiba ya Kikundi ya Absa, tutakuwa tumeweza kuiwezesha Afrika,” alisema Bi. Ndabu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi, Bw. Heristraton Genesis, alisema uzinduzi wa Akaunti ya Akiba ya Kikundi ya Absa, ambayo inaweza kufunguliwa na angalau watu watatu, ulikuwa ni mwitikio wa mahitaji ya soko.
“Tumekuwa tukipokea mapendekezo ya kufungua akaunti ya kikundi; kama taasisi ya kifedha makini, tumejibu haraka mahitaji hayo,” alisema Bwana Genesis, akibainisha kuwa akaunti hiyo ilikuwa ni mfano mseto, ikiwa na kazi za Akaunti ya Akiba ya kawaida na Akaunti ya Kikundi.
Alifafanua kuwa ili kufungua akaunti hiyo, kikundi kinapaswa kuwa na katiba, kumbukumbu za mkutano wa kuidhinisha katiba, majina ya watia saini, na barua ya utambulisho.
Alisema wamiliki wa Akaunti ya Akiba ya Kikundi ya Absa wanaanza kupata riba baada ya amana kufikia Tsh 200,000, na kwamba amana ikizidi Tsh 1,000,000, ada zote za benki zinaondolewa na inakuwa huduma ya bure.
Alibainisha kuwa akaunti hiyo ilikuwa ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kuhakikisha kuwa vikundi rasmi, na vile visivyo rasmi vyenye angalau barua ya utambulisho kutoka kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, vinapata huduma za kibenki.
“Madhumuni makuu ya Akaunti ya Akiba ya Kikundi ya Absa ni kuwawezesha watu kuunganishwa na huduma rasmi za kibenki tunapochukua hatua za kusaidia juhudi za ajenda ya ujumuishaji wa kifedha zinazoratibiwa na serikali ya Awamu ya Sita,” alisema.
Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za ya Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Heristraton Genesis (kulia), akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi rasmi wa akaunti ya akiba ya kikundi ya benki hiyo jijini Dar es Salaam leo. Wanaoshuhudia ni Meneja wa Huduma za Jamii wa Benki ya Absa, Bi. Abigail Lukuvi (kushoto), na Mkuu wa Kitengo cha Benki za Wateja Binafsi wa benki hiyo, Bi. Ndabu Lilian Swere.
Baadhi ya wanahabari wakiwa kazini wakati wa uzinduzi rasmi wa akaunti ya akiba ya kikundi ya Benki ya Absa Tanzania, jijini Dar es Salaam leo. Mkurugenzi wa Kitengo cha Benki za Wateja Binafsi wa benki hiyo, Bi. Ndabu Lilian Swere alifanya uzinduzi huo.
No comments