Shirika la USAID laipongeza serikali ya Tanzania mafanikio katika miradi ya elimu na afya nchini
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), Bwana Craig Hart (kushoto), akikabidhi mipira kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Njia Panda, Bi. Tatu Mohamedi (kulia), wakati wawakilishi wa USAID, Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) pamoja na mashirika yanayosimamia miradi inayotoa huduma kwa wagonjwa wa VVU inayofadhiliwa na mfuko huo, wakitembelea shule hiyo kuangalia maendeleo ya miradi ya USAID Kizazi Hodari Kusini, inayotekelezwa na Shirika la Deloitte shuleni hapo, Iringa, jana. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Mradi wa Kizazi Hodari, Bi. Dorothy Matoyo, Mkurugenzi Msaidizi wa USAID kitengo cha afya nchini, Bi. Anna Hofmann na Kaimu Ofisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Iringa, Samweli Mtovagakye. Ziara hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya Mfuko wa PEPFAR.
Mkurugenzi wa Mradi wa USAID Kizazi Hodari Kanda ya Kusini, Bi. Dorothy Matoyo, akitoa maelezo kuhusu mafanikio ya mradi huo unaoendeshwa na Shirika la Deloitte, wakati wawakilishi wa USAID, PEPFAR, pamoja na mashirika yanayosimamia miradi inayotoa huduma kwa wagonjwa wa VVU inayofadhiliwa na PEPFAR, wakitembelea shule ya msingi Njia Panda, kuangalia maendeleo ya afua mbili za wanafunzi wasichana ya Dreams na wavulana ya ‘coaching boys into men' (CBIM) shuleni hapo, Iringa, jana.
Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Bwana Craig Hart (katikati), akiangalia michoro inayotumika kufundishia afua za Dreams na CBIM kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Njia Panda shuleni hapo jana. Afua hizo zinahusu elimu ya uzazi, maambukizi ya VVU, tabia njema na stadi za maisha ikiwemo elimu ya kifedha. Miradi hiyo imechangia ufaulu wa shule hiyo kwa mwaka 2022, darasa la saba ufaulu ukiwa ni 97% huku darasa la nne ukiwa ni 93%.
Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Bwana Craig Hart, akisalimiana na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Njia Panda mjini Iringa, alipokwenda pamoja na ujumbe wake kukagua miradi ya USAID Kizazi Hodari Kusini inayofadhiliwa na Mfuko wa PEPFAR.
Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Bwana Craig Hart (kulia), akiagana na Mkurugenzi wa Mradi wa USAID Kizazi Hodari Kusini, Bi. Dorothy Matoyo (wa pili kushoto), mara baada ya kutembelea Shule ya Msingi Njia Panda kuangalia maendeleo ya inayosimamiwa Shirika la Deloitte kupitia mradi wa Kizazi Hodari Kusini, chini ya ufadhili wa Mfuko wa PEPFAR.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), Bwana Craig Hart (katikati), pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa USAID kitengo cha afya nchini, Bi. Anna Hofmann (wa pili kushoto), wakipiga picha ya kumbukumbu na baadhi ya mabinti wanaohudumiwa na mradi wa EpiC unaosimamiwa na Shirika la FHI360 kwa ufadhili wa Mfuko wa PEPFAR, wakati wawakilishi wa USAID na PEPFAR nchini wakifanya ziara mkoani Iringa kuangalia maendeleo ya miradi inayofadhiliwa na mfuko huo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya Mfuko wa PEPFAR. Katikati ni Mkurugenzi Msaidizi wa USAID.
Mkurugenzi wa Shirika la FHI360, Bwana Bernard Ogwang, linalosimamia mradi wa EpiC, akitoa maelezo kuhusu mafanikio ya mradi huyo katika kutoa huduma kwa wenye VVU.
Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Bwana Craig Hart (katikati kulia), akiangalia ubunifu wa kazi za mikono za mmoja wa mabinti wenye VVU wanaohudumiwa na mradi wa EpiC chini ya usimamizi wa Shirika la FHI360 mjini Iringa wakati wa ziara ya wawakilishi wa USAID, PEPFAR, mashirika yanayosimamia miradi ya USAID pamoja na waandishi wa habari kuangalia maendeleo ya miradi hiyo mkoani humo.
Na Zuhura Rashidi, Iringa
SHIRIKA la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), limeipongeza Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, chini ya Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa zinazofanyika katika kuboresha maendeleo ya miradi ya afya na elimu nchini.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la USAID, Bwana Craig Hatz, katika Shule ya Msingi Njia Panda Mkoani Iringa wakati akihitimisha ziara ya siku tatu ya wawakilishi wa shirika hilo na wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR), pamoja na mashirika yanayosimamia utekelezaji wa miradi ya ukimwi inayofadhiliwa na PEPFAR.
Akihitimisha ziara hiyo ambayo pamoja na mambo mengine ilienda pamoja na maadhimisho ya miaka 20 ya Mfuko wa PEPFAR, Bwana Hart alisema jitihada zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na USAID, PEPFAR, zimechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya miradi yote inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia USAID kwa zaidi ya miaka 60 iliyopita.
“Serikali ya Marekani kwa zaidi ya miaka 20 imewekeza zaidi ya USD Bilioni 6 nchini Tanzania, kuhakikisha tunashirikiana pamoja na serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi, wazazi na familia kukabiliana na HIV/AIDS."
“Dola bilioni 6 inaweza kuonekana nyingi, Mwaka 2000 hadi 2019 umri wa kuishi kwa mtanzania uliongezeka kwa miaka 15, ikimaanisha sasa watanzania wote wameongeza umri wao wa kuishi kwa miaka 15 zaidi, wadau wote hawa wameungana kwa ajili yako, mpo katika mazingiza bora, mnapata elimu pamoja na elimu bora ya afya, muhimu sana kwa Tanzania ya kesho, maisha yako na maisha yetu ya baadae”, alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Mradi wa USAID Kizazi Hodari Kanda ya Kusini, Bi. Dorothy Matoyo alisema wao kama Deloitte wanayo furaha kupata uwezo wa kuchangia katika maendeleo ya kizazi chenye furaha na kinachojiamini na ndipo jina lao lilipotokea.
“Kizazi tunachokiangalia sasa tunatumaini baada ya miaka 10 ama 20 ijayo kitakuwa kizazi salama chenye kujiamini, chenye upendo, kujua jinsi ya kujilinda na VVU, unyanyapaa na ukatili wa kijinsia."
“Deloitte kupitia mradi wa Kizazi Hodari Kanda ya Kusini, ni wajibu wetu kuhakikisha tunawasaidia watoto yatima pamoja na wanaoishi katika mazingira magumu katika kuwaunganisha katika vituo watakavyoweza kupata usaidizi”, alisema Bi Dorothy.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Njia Panda, Bi. Tatu Mohamedi alisema alisema shuleni hapo chini ya uratibu wa Mradi wa Kizazi Hodari Kusini, wanajishughulisha na afua mbili za ‘Dreams’ kwa wanafunzi wa kike na ‘Coaching Boys Into Men’ (CBIM) ambapo jumla ya watoto wa kike 235 na wa kiume 204 wamenufaika na mpango wa mafunzo katika afua zote mbali.
“Afua hizi zinalenga kuwasadia watoto kujitambua, kujithamini na kujiheshimu hivyo watoto hawa wamepata mafunzo kuhusu ugonjwa wa ukimwi, afya ya uzazi, ukatili wa kijinsia na kuondokana na unyanyapaa kwa wale wenye virusi."
“Miradi hii imeleta mafanikio makubwa hata kwa wanafunzi wetu kitaaluma, kupitia USAID Kizazi Hodari Kanda ya Kusini wamesaidia vifaa vya shule kama madaftari na kalamu kwa watoto wa kike 235 kwa lengo la kuwasaidia watoto hao kufanya vizuri katika mitihani yao”, alisema mwalimu huyo.
Mkurugenzi wa Shirika la FHI360, Bwana Bernard Ogwang alisema shirika lao linalosimamia mradi wa EpiC kwa ufadhili wa USAID na PEPFAR, limechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya vijana wa kike na wa kiume wanaoishi katika mazingira hatarishi ya kupata Virusi vya ukimwi.
“Katika mikoa 11 tunayohudumia, tuna idadi ya vijana wa kike na wa kiume 225 wanaopata huduma kamili ya kinga na tiba ya VVU, lakini pia vijana hawa hujishughulisha katika shughuli za kiuchumi ili waweze kuboresha maisha yao”, alisema.
Baadhi ya mabinti wenye VVU wanaopata huduma kupitia mradi wa EpiC wakitoa ushuhuda ni jinsi gani miradi ya Mfuko wa PEPFAR imeboresha maisha yao mara baada ya kugundua hali zao na kujiunga katika vituo vya huduma na tiba walisema moja ya changamoto zinazochangia kutojitokeza kwa watu wengi kupima virusi vya ukimwi ni unyanyapaa unaotokana na imani, mila potofu na kukosa elimu sahihi juu ya ugonjwa wa ukimwi.
No comments