Benki ya Absa yajizatiti katika kuwawezesha watoto wa kitanzania
Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha za Kigeni wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Esther Maruma (wa pili kulia) akikabidhi fomu baada ya kusaini makubaliano yanayoashiria makabidhiano ya msaada wa fedha kiasi cha shilingi Milioni 10 kutoka benki hiyo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na Malezi mbadala ya Watoto wenye uhitaji la SOS Children’s Villages, Bi. Dorothy Ndege jijini Dar es Salaam leo. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki yaAbsa, Bi. Nellyana Mmanyi na Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mahusiano wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Aron Luhanga.
ILI kuhakikisha watoto wa kitanzania wanafikia malengo yao ya kimaisha, Benki ya Absa Tanzania imetoa msaada wa kiasi cha Sh Milioni 10 ili kusaidia shughuli za uendeshaji wa Shirika la kimataifa linalojihusisha na malezi mbadala ya watoto lijulikanalo kama SOS Children’s Village.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya msaada huo jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa benki hiyo, Bi. Esther Maruma alisema msaada huo unaenda sambamba na lengo kuu la Benki ya Absa ambalo ni kuiwezesha Tanzania ya Kesho Pamoja, Hatua Moja Baada ya Nyingine ikiwa ni pamoja na kulikomboa Bara la Afrika Kiuchumi.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo katika hafla hiyo, Bi. Esther alisema, “Lengo la Benki ya Absa Tanzania ni kumuwezesha mtoto wa kitanzania kielimu, kiafya na kiuchumi hivyo ni imani yetu msaada huu utaleta chachu kubwa katika kuboresha maisha ya watoto wanaopata huduma mbalimbali katika kituo hiki”.
Akipokea msaada huo Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la SOS Children’s Village, Bi. Doroth Ndege alisema shirika lao litaendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama wa mtoto katika ngazi zote za jamii na hivyo kuwezesha ustawi endelevu wa jamii
“Msaada tunaoupokea utasaidia juhudi za shirika letu katika uanzishwaji wa vikundi vya hisa 210 na kugusa takribani wananchi 3150 katika mkoa wa pwani na Dar es salaam na hivyo kuboresha uchumi wao na hatimaye kuboresha malezi katika ngazi ya familia”, alisema Bi. Doroth.
Naye Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa benki hiyo, Bwana Aron Luhanga alisema benki ya Absa Tanzania imejidhatiti katika kubuni miradi mbalimbali inayolenga kuzifikia jamii zenye mahitaji na pia kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kijamii.
No comments