Breaking News

SERIKALI YAZINDUA MPANGO WA TAIFA WA KUDHIBITI UKIMWI, MAGONJWA YA NGONO NA HOMA YA INI

 

Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalim akizungumza wakati wa Uzinduzi wa mpango wa taifa wa kudhibiti ukimwi, magonjwa ya ngono na homa ya ini uliozinduliwa leo.

Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani Nchini Tanzania, Bw. Sagoe Moses akizungumza wakati wa Uzinduzi wa mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi magonjwa ya ngono na homa ya ini uliozinduliwa leo na Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalim ambae ndio alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Mratibu Mwandamizi Ofisi ya Uratibu wa PEPFAR Ubalozi wa Marekani Nchini Dk. Hiltruda Chrisant Temba akizungumza wakati wa Uzinduzi wa mpango wa taifa wa kudhibiti ukimwi, magonjwa ya ngono na homa ya ini uliozinduliwa Leo na Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalim ambae ndio alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalim pamoja na viongozi mbalimbali wakiserikali na wadau wa sekta ya afya wakikata utepe kuashiria Uzinduzi rasmi wa mpango wa taifa wa kudhibiti ukimwi, magonjwa ya ngono na homa ya ini uliozinduliwa leo jijini Dar es Salaam.



Serikali imedhamiria kutokomeza maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto pamoja na kuzuia maambukizi mapya ya ukimwi kwa kundi la vijana kuanzia umri wa miaka 15 hadi 24 kutokana na takwimu kuonyesha kuwa kundi hilo la vijana ndilo linaloathirika zaidi na maambukizi hayo.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango wa Taifa wa kudhibiti ukimwi, magonjwa ya ngono na Homa ya ini jijini Dar es salaam Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema licha ya hatua kubwa ambayo serikali na wadau wa masuala ya afya iliyopigwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi ikiwemo kupungua kwa maambukizi lakini bado makundi hayo yanahitaji nguvu zaidi katika kuyasaidia dhidi ya ugonjwa huo.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amebainisha kuwa bado kuna ongezeko kubwa la maambukizi ya magonjwa ya ngono na Homa ya Ini nchini hivyo serikali inakuja na mpango mkakati wa wa kuhakikisha kutokomeza maambukizi hayo.

Waziri ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita imeboresha huduma za afya kuanzia ngazi ya taifa hadi msingi kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya karibu zaidi na maeneo yao

“Serikali kupitia Wizara ya Afya wadau wa sekta na wataalamu wengine tayari wamefanyia kazi hoja zote zilizoibuliwa na bunge na semina zimefanyika kwa makundi mbalimbali ndani ya jamii kuhusu umuhimu wa bima za Afya kwa wote”.

“Kwa sasa nchi yetu iko mbali katika utoaji wa huduma, kuna vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa, huduma nyingi za kibingwa zinapatikana hapa hapa nchini lakini pia huduma za Afya zimesogezwa sana kwa wananchi hivyo kama serikali tuko tayari kutekeleza na kuhakikisha kuwa tunaendelea kuboresha huduma za afya kote nchini”.

Nayo baadhi ya mashirika ya kimataifa ambayo ni Shirika la La afya la Kimataifa WHO pamoja na Shirika la misaada la Marekani UNAIDS yaliyohudhuria uzinduzi huo kupitia kwa wawakilishi wao wamesifu juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dk Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muuungano waTanzania katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi na kusema wataendelea kuunga mkono juhudi hizo

No comments