WANAWAKE WAASWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIBENKI KIDIGITALI , TBA WAKIADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika katika hoteli ya Onomo jijini Dar es Salaam mapema leo, Mwenyekiti wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Taifa (NBC) Bw. Theobald Sabi alisema ni muhimu sana kwa taasisi za kifedha kuhakikisha kunakuwa na ushirikishwaji mkubwa wa wanawake kwenye huduma za kibenki au kifedha nchini.
“Tunatambua kuwa wanawake ni sehemu kubwa ya jamii yetu, zaidi ya asilimia 51 ya watanzania wote ni wanawake na kwa hivyo ni muhimu sana tunapoongeza ujumuishwaji wa kifedha kwenye jamii kundi la wanawake lisiachwe nyuma”.
Alisema Sabi. Bw. Sabi alibainisha kuwa kwa upande wa benki ya NBC wameanza na wafanyakazi wakijaribu kuhakikisha kuwa kama benki wanakuwa na sera rafiki kwa wanawake ili waweze kufikia malengo yao ya kikazi, kiajira, na kiuchumi.
Aidha naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA), Bi. Tusekelege Joune alisema kuwa inatia hamasa kuona kuwa benki nyingi nchini zimekuwa mstari wa mbele kubuni bidhaa mbalimbali ambazo zimekuwa maalum katika kukidhi mahitaji ya wanawake nchini.
“Tunashukuru kuwa benki zimekuwa mstari wa mbele katika kuja na bidhaa mbali mbali ambazo zimekuwa mahsusi kwa ajili ya wanawake hapa Tanzania. iwe mwanamke mfanyabiashara, mwanamke mtanzania, mwanamke ambaye kwa namna moja au nyingine akihitaji huduma za kibenki anakutana na bidhaa ambayo imeandaliwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake,” alisema Bi. Joune.
Bi Joune aliongeza kuwa maadhimisho haya ya Siku ya Wanawake Duniani kwa upande wa sekta ya kibenki kumekua na ongezeko kwa benki kuja na huduma ya dhamana maalum kwa ajili ya wanawake. Kutolewa kwa hati fungani kwa ajili ya maendeleo ya wanawake n.k ikiwa ni jitihada mbali mbali zinzofanywa na sekta hio katika kuinua jinsia ya kike. _____________
No comments