Halmashauri ya Jiji la Dar yaishukuru Benki ya Biashara ya DCB kusaidia sekta ya elimu
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Mhandisi Amani Mafuru (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Isidori Msaki (kulia), Diwani wa Kata ya Bonyokwa, Tumika Malilo (wa pili kushoto) na Ofisa Elimu wa jiji, Spora Tenga wakishangilia baada ya Benki ya DCB kukabidhi msaada wa madawati 30 kwa shule ya msingi Kifuru ikiwa ni sehemu ya kampeni yake inayoendelea ya elimu iitwayo “Elimu Mpango Mzima na Mama Samia”, shuleni hapo, Kinyerezi, nje kidogo kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam leo.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam (DCC) imeishukuru Benki ya Biashara ya DCB katika kusaidia uboreshaji wa elimu kwa kuchangia madawati 30 katika shule ya msingi Kifuru iliyopo Kinyerezi, Ilala nje kidogo kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa DCC Eng. Aman Mafuru amesema hayo katika hafla ya kukabidhi madawati shuleni hapo ambapo amesema tayari serikali ipo katika mchakato wa kuhakikisha shule zote za msingi zinazokabiliwa na changamoto ya madawati zinapatiwa madawati hayo.
"Tutahakikisha kwamba ushirikiano wetu na benki ya DCB Commercial Bank unasonga mbele katika kuhakikisha kuwa tunatatua changamoto nyingi za huduma za kijamii zinazoikabili manispaa na jamii kwa ujumla," alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Isidori Msaki, alisema katika jitihada za kuisaidia Serikali ya Tanzania kuboresha sekta ya elimu nchini, benki ya Biashara ya DCB ina mpango wa kuchangia angalau madawati 1,000 katika shule mbalimbali za msingi nchini kati ya mwaka 2023/2025.
Msaki alisema madawati 30 yanayotolewa katika Shule ya Msingi Kifuru iliyopo Kinyerezi, Ilala, Dar es Salaam ni miongoni mwa madawati 150 ambayo benki hiyo itasaidia shule mbalimbali za msingi za Manispaa ya jiji hilo.
Alisema pamoja na kuboresha sekta ya elimu, madawati hayo pia yatahakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri, hivyo kusaidia kuboresha ufaulu wa wanafunzi katika shule za sekondari.
"Tunaunga mkono kampeni yetu iliyopewa jina la 'Elimu Mpango mzima na Mama Samia' inayotambua umuhimu wa elimu katika maendeleo ya taifa," alisema.
Msaki alisema kupitia Bodi ya wakurugenzi ya Benki ya DCB inayoongozwa na Bi Zawadia Nanyaro inalenga kuhakikisha kuwa wanafunzi wa shule za msingi wanakuwa na mazingira mazuri ya kujifunzia.
Alisema benki hiyo pia inaunga mkono mipango ya manispaa katika kuboresha sekta ya elimu mkoani humo na nchi nzima kwa ujumla ambapo katika hafla hiyo benki inakabidhi madawati 30 kati ya 150 yaliyopangwa kukabidhiwa kwa halmashauri za manispaa ya Dar es Salaam.
"Tunaamini serikali kupitia kwa Rais Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kubwa kuboresha sekta ya elimu, lakini serikali pekee haiwezi kumudu gharama zote za elimu kwa wanafunzi nchini," alisema.
Alisema benki hiyo itaendelea kusaidia mipango mbalimbali ya maendeleo ya serikali katika sekta ya elimu katika shule hiyo inayokabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo majengo ya madarasa, vyoo, madawati pamoja na huduma nyingine za kijamii katika shule hiyo na nchi nzima kwa ujumla.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Mhandisi Amani Mafuru ( kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Isidori Msaki wakikata utepe kuashiria makabidhiano ya msaada wa madawati 30 kwa shule ya msingi Kifuru yaliyotolewa na DCB ikiwa ni sehemu ya kampeni yake inayoendelea ya elimu iitwayo “Elimu Mpango Mzima na Mama Samia” jijini leo. Wengine kutoka kushoto ni Ofisa Elimu kata ya Bonyokwa, Sylvia Lyimo, Ofisa Elimu wa jiji, Spora Tenga, Diwani wa Kata ya Bonyokwa, Tumika Malilo na Mkuu wa Shule ya Kifuru, Wilfred Lwagaza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Isidori Msaki akishikana mikono na wanafunzi wa shule ya msingi Kifuru baada ya kuwakabidhi msaada wa madawati 30 kama sehemu ya kampeni yake inayoendelea ya elimu iitwayo “Elimu Mpango Mzima na Mama Samia” jijini leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Isidori Msaki akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa madawati 30 kwa shule ya msingi Kifuru shuleni hapo, Kinyerezi nje kidogo kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam leo.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Mhandisi Amani Mafuru akizungumza kabla hajapokea msaada wa madawati 30 yaliyotolewa na Benki YA DCB, shuleni hapo, Kinyerezi, Dar es Salaam leo.
Diwani wa Kata ya Bonyokwa, Tumika Malilo akizungumza katika hafla hiyo jijini Dar es Salaam leo.
Mkuu wa Mawasiliano na Masoko wa Benki ya Biashara ya DCB, Rahma Ngassa akipiga picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Kifuru mara baada ya hafla hiyo, shuleni hapo leo. DCB ilikabidhi msaada wa madawati 30 yakipokewa na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Mhandisi Amani Mafuru.
Mkuu wa Shule ya Msingi Kifuru akitoa neno la shukrani baada ya Benki ya Biashara ya DCB kukabidhi madawati 30 kwa shule yake kupitia kampeni yake inayoendelea ya elimu iitwayo “Elimu Mpango Mzima na Mama Samia”. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Isidori Msaki, Ofisa Elimu wa jiji, Spora Tenga, Diwani wa Kata ya Bonyokwa, Tumika Malilo na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Mhandisi Amani Mafuru.
No comments