WAZIRI JAFO AIPONGEZA TBS KUBORESHA UTOAJI WA TUZO ZA UBORA
Na Mwandishi Wetu.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Selemani Jafo (Mb) ametoa rai kwa Wazalishaji wa bidhaa Nchini kuweka kipaumbele suala la ubora wa bidhaa kwani ndio ajenda muhimu kwa kutengeneza uchumi wa nchi.
Ameyasema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Ubora Duniani na Utoaji wa Tuzo za Kitaifa za Ubora kwa washindi wa msimu wa tano 2024 yaliyofanyika katika ukumbi wa PSSSF Tower Jijini Dar es Salaam.
Dkt.Jafo ameyataka makampuni mbalimbali kujua kuwa mashindano hayo yanalenga kuchochea uzalishaji wa bidhaa kwa kuzingatia ubora ili kuweza kufikia viwango vya masoko ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.
Aidha amesema kuwepo kwa vyakula na vifaa mbalimbali vinavyokosa ubora husababisha madhara makubwa kwa kutengeneza watu wenye magonjwa pamoja na madhara kwenye miundombinu mikubwa inayotumia vifaa vya ujenzi ambavyo havina ubora.
Pia ametoa rai kwa Wajasiliamali kutumia fursa kujenga biashara na ujasiliamali wao ili wakue na kuanza kutengeneza bidhaa zinazokidhi Viwango kwani fursa iliyopo ni wajasiliamali wadogo wanalelewa na SIDO na ndani ya miaka mitatu husaidiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) bila gharama.
Pamoja na hayo Dkt.Jafo amewataka watanzania wawe na tabia ya kutumia bidhaa za ndani kwani uwekezaji wa viwanda umekuwa mkubwa na bidhaa nyingi zinazalishwa nchini na kwakufanya hivyo inahamasisha uwekezaji kuwa mkubwa.
Vilevile ameliagiza Shirika la Viwango Tanzania kujenga uelewa na kuitangaza siku hiyo ya Viwango kwa kiasi kikubwa zaidi kwa Watanzania ili kuwa na idadi kubwa ya washiriki kwenye tuzo zijazo katika vipengele tofauti.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo hizo, Cresensia Mbunda, amesema kila mwaka Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia TBS na ZBS wakishirikiana na sekta binafsi wamekuwa wakiandaa tuzo za ubora.
Amesema wanafanya hivyo kama sehemu ya kuhamasisha matumizi ya viwango vya ubora na ushindani katika sekta mbalimbali nchini na kutambua na kuthamini juhudi za wazalishaji waliofanya vizuri kwa mwaka.
Pamoja na hayo amesema timu ya majaji saba kutoka sekta binafsi na serikali walipitia na kuchakataa maombi 52 yaliyokusanywa kwenye kuwania tuzo hizo bila upendeleo wowote na kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi amewapongeza washiriki wote na kuwasisitiza kuendelea kuzalisha bidhaa zinazokidhi ubora ili kutanua wigo wa biashara kimataifa.
Amesema tuzo hizo zinafanyika ikiwa ni msimu wa tano zikiwa na lengo la kuwatambua na kuwapongeza watu binafsi pamoja na taasisi zinazofanya vizuri kwenye masuala ya ubora wakati wa utekelezaji wa shughuli zao za uzalishaji bidhaa au utoaji huduma.
"Lengo jingine kufanyika kwa tuzo hizi ni kuhamasisha ubunifu na uboreshaji wa bidhaa na huduma zinazotolewa hapa nchini kupitia taratibu zilizowekwa chini ya miundombinu ya ubora". Amesema Dkt. Katunzi.
Hata hivyo Dkt. Katunzi amesema katika zama hizi tulizopo ni ngumu kuzuia bidhaa na huduma kutoka kwenye nchi moja kuuzwa kwenye nchi nyingine kutokana na uwepo wa kanuni za kimataifa hususani kanuni za WTO zinazozuia kuweka vikwazo vya kiufundi kwenye biashara yaani WTO Technical Barrier to Trade Agreement.
"Kwa sababu hiyo njia bora ya kulinda soko la bidhaa na huduma zetu ndani na nje ya mipaka yetu ni kuzalisha bidhaa na kutoa huduma zenye ubora wa hali ya juu na kwa gharama nafuu". Ameeleza.
WAZIRI JAFO AIPONGEZA TBS KUBORESHA UTOAJI WA TUZO ZA UBORA
Reviewed by Adery Masta
on
23:22
Rating: 5
No comments