TCB WAJA NA POPOTE AKAUNTI WARAHISISHA KULIPIA TIKETI ZA SGR , BILI ZA MAJI , LUKU , MALIPO YA KISERIKALI NA KUTUMA PESA POPOTE
Na Adery Masta.
Watanzania wanatarajia kunufaika na huduma mpya ya kidijiti inayotolewa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) ambayo imetambulishwa kwa chapa ya Popote Account lengo likiwa ni kuwafikia wananchi zaidi na kutimiza kile kinachoitwa ujumuishi wa kifedha.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Masoko, Ukuzaji wa Biashara na Mahusiano ya Umma wa TCB Deo Kwiyukwa akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne Julai 30, 2024 wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo uliofanyika Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Dar es Salaam.Amesema kwamba benki ya TCB wameamua kuwa benki yenye ubunifu kwa muda mrefu akikumbusha huduma waliyoizindua miezi michache iliyopita ya Toboa na Kikoba ambapo walijiunga na kampuni zote kubwa za simu, hivyo huduma mpyaimetajwa kuwa mwendelezo wa benki hiyo kukidhi mahitaji ya wananchi.
"Kwenye ile huduma yetu mpya tumeweza kuongeza vionjo vingi, mtu anaweza kupata huduma zote za kibenki ikiwamo kulipia bili mbalimbali, na kikubwa kama mnakumbuka hivi karibuni tumezindua uuzaji wa tiketi tukishirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC), sasa hii huduma itamuwezesha pia mteja wetu mwenye hiyo akaunti kupata huduma ya tiketi" Ameeleza Kwiyukwa.Amesema katika huduma hiyo mpya inayopatikana katika programu tumizi ya Tanzania Commercial Bank (TCB), mteja hahitaji kwenda hatua nyingine kwenye ununuzi wa tiketi za treni ya mwendokasi baada ya kuwa tayari kanunua kwa kuwa atapewa msimbomilia yaani QR Code itakayomuwezesha kusomeka kwenye magati ya treni.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Huduma za Kidijiti na Ubunifu wa TCB Jesse Jackson amesema kwamba TCB ikiwa ni benki ya tatu kwa ukubwa wa Kimatawi Tanzania na ikiwa na Mawakala zaidi ya 6000 bado inaona ni muhimu kwa Watanzania zaidi kuendelea kufikiwa na huduma za kifedha.
"TCB kama benki inayomuelewa Mtanzania zaidi, leo hii tumewaletea huduma hii ya Popote Account ambayo Mtanzania au mteja yeyote anaweza kuifungua mahali popote alipo kwenye simu yake janja na anachohitaji ni kitambulisho au namba yake ya NIDA na anaweza kufungua akaunti hii na akifuata maelekezo ndani ya dakika mbili anaweza kujipatia akaunti hiyo" Ameeleza Jesse.Amesema anaweza kupata huduma mbalimbali ikiwamo kulipia bili, malipo ya serikali, kupata mikopo na huduma nyingine zinazoweza kumpatia Mtanzania masuluhisho ya kifedha.
" Tunawasihi Watanzania waendeleee kutumia huduma zetu na tunawashukuru sana kwa kutuamini TCB katika kuwapatia huduma zao za kifedha" Ameeleza Jesse.
No comments