Wafanyakazi wa Benki ya NBC wajitolea damu kusaidia wenye mahitaji
Ofisa Fedha Mkuu wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Waziri Barnabas (katikati), akihojiwa na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, wakati yeye na mwenzake, Fanuel Jenga (kushoto), wakijitolea damu katika zoezi lililoandaliwa na benki hiyo kwa wafanyakazi wake kujitolea damu kusaidia wenye mahitaji kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama.
Ofisa Fedha Mkuu wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Waziri Barnabas (kulia), pamoja na Mhasibu wa benki hiyo, Fanuel Jenga (kulia kwake) wakichukuliwa vipimo vya damu kabla ya kujitolea damu jijini Dar es Salaam leo, katika zoezi liloandaliwa na benki hiyo kwa wafanyakazi wake pamoja na wakazi wengine wa jiji hilo kusaidia wenye mahitaji kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama. Kushoto ni Evelyn Dielly kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama.
Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) wakijitolea damu katika zoezi liloandaliwa na benki hiyo kwa wafanyakazi wake pamoja na wakazi wengine wa Jiji la Dar es Salaam leo kujitolea damu kusaidia wenye mahitaji kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama.
Mkazi wa Chalinze, Joshua Mjuni akijitolea damu katika zoezi liloandaliwa na NBC kwa wafanyakazi wake pamoja na wananchi wengine leo, kujitolea damu kusaidia wenye mahitaji kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama. Anayemhudumia ni muuguzi kutoka Damu Salama, Peter Chami.
Ofisa Uhamasishaji wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Fatuma Mjungu, akihojiwa na waandishi wa habari katika zoezi la uchangiaji damu wa hiari lililkoandaliwa na Benki ya NBC jijini Dar es Salaam leo.
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Watanzania wamehimizwa kushiriki zoezi la kuchangia damu kwa hiari ili kukidhi mahitaji makubwa ya damu na kuokoa maisha ya wenzao pamoja na kusaidia huduma za afya nchini.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Ofisa Fedha Mkuu wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Waziri Barnabas akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Bbenki hiyo, Theobald Sabi wakati wa tukio la kuchangia damu kwa hiari lililondaliwa na NBC akisema kwamba huo ni utamaduni wa benki hiyo wa kuchangia damu kwa kujitolea.
Alisisitiza kwamba ni muhimu kwa watanzania kuanza kujitokeza na kujitolea damu kwa hiari ili kuendelea kuokoa maisha ya wenye mahitaji.
"Hii ni mara ya tatu kwa benki hii na wafanyakazi wake kushiriki kwenye kampeni ya uchangiaji damu ili kuokoa maisha ya wakinamama wanaojifungua, waliopata ajali na watu wengine wenye mahitaji ya damu nchini,” aliongeza.
Barnabas aliongeza kwamba kwamba mahitaji ya damu bado yapo juu kwenye mahospitali hasa kwenye upasuaji na bado mwamko upo chini kwa wananchi kama uchangiaji wa damu kwa hiari.
"Ni muhimu sana kwa watanzania wenzetu kuungana nasi katika shughuli ya kujitolea ya kuchangia damu ambayo inatarajiwa kumalizika kesho,” alisema.
Alisema kwamba kwenye shughuli hiyo wanatarajia kukusanya takriban chupa 100 kutoka kwa wafanyakazi wa benki hiyo na watu wengine kutoka maeneo mbalimbali ya jiji ili kupunguza mahitaji makubwa ya damu nchini na alisisitiza kuwa kampeni hiyo inapaswa kuwa endelevu kukidhi matarajio ya nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Rasilimali watu wa benki hiyo, Grace Mgondah alisema kwamba wanatarajia wafanyakazi 500 kutoka kwenye matawi mbalimbali watashiriki katika zoezi hilo la siku mbili ya kujitolea damu kwa hiari.
"Hii ni sehemu ya huduma kwa jamii ambayo benki yetu ya NBC inasikia fahari kuwahudumia na ninatoa wito kwa watanzania wenzetu kujitokeza kwa wingi kuja kutuunga mkono,” alisisitiza.
Fatuma Mjungu kutoka Kitengo cha Taifa cha Damu Salama (NBTS) alisema kwamba mwaka huu wanatarajia kukusanya chupa 450,000 za damu kutoka kwenye taasisi mbalimbali na watu wanaojitolea kwa hiari.
"Mahitaji ya damu kwa sasa nchini ni chupa 520,000 lakini asilimia moja tu ya watanzania wote wakichangia damu tunaweza kukidhi mahitaji ya damu kwa taifa,” aliongeza
Mjungu pia ametoa wito kwa taasisi na makampuni nchini kuinga mkono benki hiyo ya NBC kwa kuhamasisha wafanyakazi wake na wananchi wengine kwa ujumla kujitolea damu kwa ajili ya watu wenye uhitaji.
No comments