Breaking News

Jinsi uhaba wa wakalimani wa lugha ya alama unavyoathiri wanawake viziwi

Wanawake viziwi na wanachama wa chama cha wanawake viziwi (FUWAVITA) wakisherehekea wakati wa mahadhimisho ya Wiki ya Wiziwi duniani yalifanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni. (Picha na Mpiga Picha Wetu). 
Wanawake nchini wanakabiliwa na matatizo mengi sana kama vile ukatili wa kijinsia, unyanyasaji wa kingono na aina nyingine za unyanyasaji kuanzia ngazi ya familia hadi ya taifa. “Lakini wanaoathirika zaidi ni wanawake viziwi kwani haki zao mara nyingi zinakandamizwa,” anasema mtaalamu wa ustawi wa jamii, Bi Heldina Mwingira.
Umaskini, kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu ni miongoni mwa sababu kubwa zinazofanya wanawake viziwi wakose haki zao. Vyanzo mbalimbali kutoka serikalini, kama vilivyoripotiwa na vyombo vya habari, vinaonyesha kwamba takriban asilimia 55 ya wanawake viziwi nchini hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu, wengi wao ni maskini.
“Uhaba wa wakalimani wa lugha ya alama unaongeza tatizo kwa wanawake viziwi kukosa msaada wa sheria na haki katika vyombo mbalimbali vinavyotoa haki,” anaongeza Bi Mwingira, anayefanya kazi na Shirikisho la Wanawake Viziwi, Dar es Salaam. Kwa sasa kuna wakalimani wa lugha ya alama wapatao 28 tu Tanzania, ambapo idadi hii ni ndogo sana ukilinganisha na mahitaji yaliyopo sehemu mbalimbali nchini.
“Wanawake viziwi wanakosa haki mahakamani, vituo vya polisi, ofisi za Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na ustawi wa jamii kutokana na shida ya mawasiliano kwa vile wote - watafuta huduma (wanawake viziwi) na watoa huduma - wanakabiliwa na changamoto ya kutojua lugha ya alama,” anasisitiza.
Ili kukabiliana na tatizo hili na kuwasaidia wanawake viziwi kutatua matatizo yao ya kisheria, Shirikisho la Wanawake Viziwi, the Joy of Deaf Women Entrepreneurs Tanzania (FUWAVITA), limechukua hatua mahsusi kwa kuweka utoaji wa msaada wa sheria kwenye mipango yake ili kuwasaidia wanawake viziwi kupata haki.
Hivi karibuni, FUWAVITA iliadhimisha Wiki ya Kimataifa ya Viziwi yenye dhamira “Haki ya Kutumia Lugha ya Alama ni Suluhisho kwa Utoaji wa Msaada wa Sheria kwa Wanawake Viziwi Tanzania’’.
“Kuchagua dhamira hii kulikuwa na lengo la kupeleka ujumbe dhahiri kwa jamii kubwa ya Watanzania juu ya umuhimu wa lugha ya alama kama kweli tunataka mamilioni ya wanawake viziwi kutatua matatizo ya kisheria sehemu mbalimbali nchini,” anasema Bilbosco Muna, ambaye ni mkalimani anayefanya kazi na FUWAVITA.
Wiki ya Kimataifa ya Viziwi, iliyofanyika kwenye viwanja vya Mwananyamala jijini Dar es Salaam Septemba 23-28, 2019, ilidhaminiwa na LSF, ambalo ni shirika lisilo la kiserikali na linalofanya kazi isiyozalisha faida. Shirika hili linalotoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na yanayotoa msaada wa sheria Tanzania.
Kwa ujumla, Wiki ya Kimataifa ya Viziwi ilihudhuriwa na zaidi ya watu 1,000—ikiwa ni pamoja na watu wa kawaida, wanawake viziwi, mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo, maofisa wa ustawi wa jamii kutoka halmashauri za manispaa za Dar es Salaam—Temeke, Ilala, Kinondoni na Ubungo—yenye lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu mtu kuwa kiziwi, hasa sababu zinazofanya watu kuwa hivyo, kiwango chake, aina yake, vipimo vinavyofanyika kuona kama mtu ni kiziwi au la na mambo mengine.
Lengo lilikuwa hasa kutoa elimu kwa wanasheria, maofisa wa ustawi wa jamii, mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo na wanawake viziwi kuhusu utumiaji wa lugha ya alama. Sababu kubwa ya kufanya hivi ilikuwa kurahisisha mawasiliano kati ya watoa huduma (mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo, wanasheria na maofisa wa ustawi wa jamii) na wanawake viziwi ili kuelewa zaidi matatizo yanayowapata na namna ya kuwasaidia kuyatatua na hivyo kupata haki zao.
Pamoja na kuwafanya watoa huduma kujua mambo ya msingi kuhusu lugha ya alama, FUWAVITA inapanga kwenda mbali zaidi kwa kuanzisha mafunzo maalumu kwa ajili ya wasaidizi wa kisheria viziwi (wanaume na wanawake) watakaoenda sehemu mbalimbali nchini kutoa msaada wa sheria kwa wanawake wengine viziwi.
Kwa sasa, kuna zaidi ya wasaidizi wa kisheria 4,000 walioandikishwa kupitia fedha zilizotolewa na LSF kutoa msaada wa sheria kwa jamii, lakini wengi wao hawajui kusoma lugha ya alama.
“Ili kuwasaidia wanawake viziwi kutatua matatizo yao, wasaidizi wa kisheria wanahitaji wakalimani, lakini wengi wa wanawake hao hawawezi kumudu gharama zao…kuna matukio mengi yaliyokwisha ripotiwa ya wanawake viziwi ambao wameshindwa kesi zao, wamenyanyaswa, wamepoteza mali, wametalakiwa, baadhi wamefukuzwa kutoka kwenye nyumba/ardhi na kunyimwa haki zao kwa sababu ya tatizo la mawasiliano na kushindwa kupata mkalimani wa lugha ya alama kutokana na kutomudu gharama,” anasema Bi Anet Gerana Isaya, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa FUWAVITA.
Kwa mujibu wa Bi Isaya, mafunzo ya wasaidizi wa kisheria viziwi yatafanyika sambamba na mafunzo ya mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo, maofisa wa ustawi wa jamii na wanawake viziwi wenyewe walioko Dar es Salaam kuhusu utumiaji sahihi wa lugha ya alama Tanzania.
Hii itaondoa gharama zisizo za lazima za kuwalipa wakalimani wa lugha ya alama na kurahisisha mawasiliano linapokuja suala la kushughulikia kesi za wanawake viziwi kwa vile wahusika wote—mahakimu, maofisa wa hifadhi ya jamii, wasaidizi wa kisheria viziwi na wanawake viziwi watakuwa wakitumia lugha moja, anasema mkurugenzi mkuu wa FUWAVITA.
Anaeleza kwamba “tofauti na ilivyokuwa hapo zamani, kutakuwa pia na faragha/usiri katika kushughulia kesi zinazohusu wanawake viziwi na kuwafanya waweze kujieleza kwa uhuru zaidi. Mwisho wa siku, kesi zinazowahusu wanawake viziwi zitashughulikiwa kwa haki zaidi katika mfumo rasmi na usio rasmi na kuwawezesha kupata haki,” anasema Bi Isaya.
Akitoa maoni yake, mtaalamu wa hifadhi ya jamii Bi Heldina Mwingira, amesema “uandikishaji wa wasaidizi wa kisheria unarahisisha utoaji wa haki kwa wakati kwa wanawake viziwi wenye matatizo ya kisheria na matatizo mengineyo.” Kwa mujibu wa FUWAVITA, uandikishaji wa wasaidizi wa kisheria utaanza na kata za Dar es Salaam na baadaye mikoani kwa kutegemea ufanisi wa mradi awamu ya kwanza.

No comments