Breaking News

Benki ya NBC yajipanga kutoa huduma bora msimu mpya wa ununuzi wa korosho Mtwara

Ofisa Huduma Wateja wa Benki ya NBC Tawi la Mtwara, Lulu Mutayoba (katikati), akitoa maelezo kuhusu huduma za kibenki zotolewazo na NBC kwa watu waliotembelea banda lao wakati wa Kongamano la Uwekezaji na Maonyesho ya Biashara Mtwara yaliyofanyika katika Viwanja vya Chuo cha Elimu Mtwara mwishoni mwa wiki. 
Wakulima wa Korosho kuufaika na huduma za NBC msimu mpya wa ununuzi wa zao hilo.
Na Mwandishi wetu,Mtwara
WAKATI wakulima wa korosho wakiendelea na msimu mpya wa korosho kwa mwaka 2019/20 Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesema itaendelea kuwahudumia na kuwahakikishia usalama wa fedha zao huku ikisogeza huduma hizo karibu zaidi badala ya kusafiri umbali mrefu.

Akizungumza wakati wa Kongamano la Uwekezaji na Maonyesho ya Biashara mkoani Mtwara mwishoni mwa wiki, Meneja wa NBC Mkoa wa Mtwara, Job Nshatsi alisema wameendelea kuwa mstari wa mbele kutuoa huduma za kibenki, ushauri na mafunzo ya kifedha na biashara yanayowezeha wateja wake ikiwemo wakulima na wafanyabiashara wa korosho.

Alisema katika kuhakikisha wakulima wananufaika na huduma zake tayari wameendelea kuongeza mtandao wao wa mawakala katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wakulima wanapata fedha kwa wakati lakini pia kwa usalama kwa kuepuka kusafiri na fedha umbali mrefu kwenda palipo na tawi la benki hiyo.

“NBC tunatoa huduma za kibenki maalumu kwa ajili ya kukuza na kuendeleza kilimo-biashara (agribusiness) kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi ya Kilimo nchioni (PASS), tukiangalia sekta ya kilimo na mnyororo mzima wa thamani katika kilimo, na kwa Mtwara tutaendelea kutoa huduma ili kusaidia kukuza uzalishaji, uongezaji wa thamani na uuzaji wa zao la korosho,”alisema Nshatsi

Aidha alisema NBC kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) wanaendelea kutoa elimu za kifedha kwenye vikundi mbalimbali vya wajasiriamali lengo ikiwa ni kuwawezesha wajasiriamali hao kupata mbinu mbalimbali katika kuendesha biashara zao.

Nshatsi alizidi kueleza kuwa ili kuhakikisha watu wengi wanafikiwa na huduma za kibenki wamerahisisha ufunguaji wa akaunti kupitia akaunti ya NBC Fasta ambapo mteja anahitajika kuwa na kitambulisho kimoja au barua ya mtendaji na kufunguliwa akaunti.

Wakizungumza baadhi ya wananchi waliohudhuria kongamano hilo waliziomba taasisi za kifedha kuendelea kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya fedha hasa katika kipindi hiki cha msimu wa mavuno ya korosho.

“Tunapohudhuria makongamano tunatumaini tutapata elimu mbalimbali lakini watu wa benki waendelee kutoa elimu ya matumizi sahihi ya  fedha ili kuwa endelevu hasa kipindi hiki ambacho wakulima wanauza korosho wasaidiwe wajue baada ya kuuza fedha wanazozipata wanatakiwa kuziendeleza kwenye miradi mingine ya maendeleo,”alisema Asha Chimae

Naye mwanachi mwengine Hansi Chilumba alisema “Wananchi wapo tayari kufanya kazi lakini kinachokosekana ni ujuzi na mtaji, ni vizuri benki kuendelea kutuwezesha hata mmoja mmoja ili kutimiza malengo kwa sababu kila mtu anakuwa na malengo yake lakini tunapounda kikundi inakuwa ngumu kwa wote kukubali wazo la mmoja ili kulifanyia kazi.

No comments