Breaking News

WABUNGE WANAWAKE, ORYX WAMPA TUZO RAIS DK. SAMIA

Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas kama Benoit Araman (wanne kushoto), akisoma ujumbe uliondikwa katika Tuzo ya Rais Samia Suluhu Hassan iliyotolewa na Kampuni hiyo kwa ajili ya kutambua mchango wa Rais katika kuhimiza matumizi ya Nishati Safi ya kupikia.Tuzo hiyo imepokelewa na Spika wa Bunge Dk.Tulia Ackson leo wakati wa Mashindano ya Siku ya Nishati Safi ya Kupikia Duniani ambapo kwa Tanzania Oryx wameshikiana na Wabunge wanawake kuadhimimisha siku hiyo

WABUNGE wanawake nchini kwa kushirikiana na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania wametoa tuzo kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kutambua mchango wake katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Tuzo hiyo kwa Rais Dk. Samia imetolewa leo Juni 7, 2024 Mjini Dodoma wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Nishati Safi ya Kupikia Duniani ambapo Oryx, wabunge wanawake, wabunge vinara katika nishati safi wametumia maadhimisho hayo kujadili kwa kina mchango wa Rais Dk. Samia katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia Afrika, hususan Tanzania.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson aliyekuwa mgeni rasmi, amesema kuna kila sababu kwa wabunge na Oryx kumpa tuzo Rais Dk. Samia kwa kuwa amekuwa kinara wa nishati safi ya kupikia na juhudi zake zinashuhudiwa na Watanzania, Afrika na dunia kwa ujumla.

Amesema Rais Samia alipokuwa nchini Dubai na hivi karibuni aliposhiriki mkutano kuhusu nishati safi ya kupikia Paris, Ufaransa ametambuliwa kuwa kinara wa nishati hiyo.
Hivyo wanaendelea kusisitiza Dk. Rais Samia ndiye kinara wa nishati safi ya kupikia.

Amesema katika Bara la Afrika kunachangamoto ya nishati ya kupikia na takwimu zinaonesha asilimia 80 ya wananchi barani humo wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia na kwamba kutoka katika nishati hiyo itachukua muda. 

“Hivyo Rais Dk. Samia anasaidia kupunguza muda kwa kuendelea kutafuta fursa kubadilisha upikaji kwa kuacha kutumia nishati chafu na kuhamia katika nishati safi ya kupikia kama gesi.

“Juhudi hizo za Rais zimeanza Tanzania na takwimu nchini zinaonesha asilimia 90 ya wananchi hadi sasa wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia.

“Hivyo juhudi za Rais zinatusogeza angalau kutoka asilimia 90 na kusogea hadi 25 ili wawe wachache wanaotumia nishati chafu ya kupikia,” amesema.

Akifafanua zaidi Dk. Tulia amesema wanafahamu nishati isiyo safi ina madhara kwa binadamu na kwa nchini takwimu zinaonesha vifo takribani 33,000 hutokea kila mwaka kutokana na athari za kutumia nishati isiyofaa, hivyo kupoteza nguvu kazi ya taifa.

Amesema mbali na vifo, kutumia nishati chafu kumekuwa kukisababisha athari za mazingira na kijamii huku akitumia nafasi hiyo kueleza namna ambavyo wanawake na mabinti wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta kuni na mkaa badala ya kufanya shughuli za maendeleo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amesema kwa kutambua mchango wa Rais Samia katika nishati safi wameamua kumpa tuzo kumuunga mkono juhudi zake za kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.

Benoit amesema tuzo hiyo ina ujumbe usemao “Kampuni ya Oryx Energies inatoa tuzo hii kwa Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutambua uongozi wake wa kipekee katika kushinda na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania na Afrika.”

Akitoa ahadi ya kampuni hiyo, amesema hadi sasa wameshatoa mitungi ya gesi na majiko yake 35,000 kwa makundi mbalimbali nchini na wataendelea na mkakati wao kwani dhamira yao ni kuona asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2032 inafikiwa kama ambavyo Rais Samia ameelekeza.

Awali Mwenyekiti wa Wabunge Wanawake nchini Shally Raymond, amesema wabunge wanawake pamoja na wabunge vinara wa nishati kwa kushirikiana na Oryx wameamua kutoa tuzo kwa Rais huku akitumia nafasi hiyo kupongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia nchini.

No comments