Breaking News

WANAWAKE DIT WAWATEMBELEA NA KUWAPA ZAWADI WENYE MAHITAJI MAALUM

 Na Mwandishi Wetu.

Wanawake wa Taasisi ya Teknolojia Dar-es-salaam (DIT) wameadhimisha siku ya Wanawake Duniani kwa shughuli za kijamii ikiwemo kutembelea kituo cha mazoezi cha watoto wenye mahitaji maalum  cha Hezron kilichopo Keko Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam na kuwapatia zawadi za vifaa mbalimbali.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo katika kituo hicho, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa DIT Bi. Agnes Kimwaga alisema DIT inawakumbuka wahitaji wakati wote na kipindi hiki imeona ni vyema kuwatembelea watoto wenye mahitaji maalum.

"Tumeona ni vyema  tulete zawadi hizi kwa wahitaji kwa sababu  watoto wana mahitaji mengi  na tunaamini vifaa tulivyokabidhi vitasaidia na kuwapa faraja wamama ambao mnajukumu kubwa la kulea watoto hawa".

"Hii ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani , sisi kama wamama tunajali na tumeona ni muhimu kuwatembelea watoto hawa na kuwasaidia wanawake wenzetu kuanzia kwenye ngazi ya familia na jamii yote kwa ujumla", alisema Bi. Kimwaga.

Akipokea zawadi hizo, Fatuma Iddi ambaye ni mmoja wa wamama wa watoto wenye mahitaji alisema wameshukuru kwa zawadi zilizotolewa na DIT huku akiomba kuendelea kuwa kumbuka zaidi makundi haya maalum.

"Tunashukuru kwa zawadi hizi na tumefurahia kwa sababu watoto hawa wana mahitaji na changamoto nyingi kutokana na uhitaji wao ". Selina Saimon Ngaina aliongeza kwa kusema

"Kuna uhitaji mkubwa wa eneo kwa sababu linahitajika eneo kubwa la kufanyia mazoezi  watoto  hapa ni padogo, lakini pia watoto wanatoka mbali wakati mwingine wazazi wanashindwa kuwaleta watoto kutokana na kukosa nauli, hivyo niwaombe wadau mbalimbali kujitokeza ili tuweze kupata eneo pia namna ya  kuwasaidia wamama hawa juu ya gharama ya kuleta watoto mazoezi".

DIT imekabidhi zawadi mbalimbali ikiwemo sabuni za unga, mafuta ya kupaka , pampasi, siagi na sukari.

No comments