BENKI YA DCB YAZINDUA PROGRAMU YA VICOBA KUBORESHA MAISHA YA WATANZANIA
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara DCB, Bwana Sabasaba Moshingi (wa pili kulia), akizungumza wakati wa uzinduzi programu ya DCB Vicoba pamoja na uzinduzi wa mradi wa kumiliki Coaster 5 wa Umoja wa Vikundi vya Ujasiriamali Kivule (UVUKI) uliopo chini ya Shirikisho la Vikundi vya Ujasiriamali Tanzania (SHIVUTA), uliofanyika Kitunda, Ilala, nje kidogo kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam leo.
KATIKA kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha huduma za Kifedha zinawafikia watu wengi, kirahisi na gharama nafuu, Benki ya Biashara ya DCB imezindua programu ya VICOBA ikiwalenga wateja wa Vicoba na makundi mengine ya kijamii.
Uzinduzi wa DCB VicobaApp umefanyika Kitunda, Ilala nje kidogo ya jijini Dar es Salaam leo sambamba na hafla ya uzinduzi wa mradi wa kumiliki Coaster tano ulioandaliwa na Umoja wa Vikundi vya Ujasiriamali Kivule (UVUKI), chini ya Shirikisho la Vikundi vya Ujasiriamali Tanzania (SHIVUTA).
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Bwana Sabasaba Moshingi alisema programu hiyo itawawezesha wanachama wa vicoba kufanya miamala yao kwa urahisi na usalama zaidi, hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii.
“Tunatambua umuhimu wa teknolojia katika kuboresha maisha ya watu, na ndio maana tumeamua kuja na DCB VicobaApp ili kusaidia wanachama wa vikoba na makundi mengine ya kijamii kupata huduma za kifedha kwa urahisi zaidi kupitia simu zao za mkononi.
“Ikianzishwa takribani miaka 22 iliyopita kupitia wito wa Rais Mstaafu Hayati Benjamin William Mkapa, kipaumbele chetu kikubwa kimekuwa ni kuinua maisha ya watanzania wenye kipato cha wastani kiuchumi, hususan wajasiriamali wadogo na wa kati lakini tukiangaza zaidi kwa watanzania ambao mara kadhaa wamekuwa wakikosa vigezo vya kupata mikopo na urahisi wa kuwekeza katika benki za kibiashara,” alisema Bwana Moshingi.
Ni katika muktadha huo Bwana Moshingi alisema, DCB imekuwa mwanzilishi na kuwa kinara katika kuanzisha huduma za mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo, wateja binafsi na kwa vikundi vya Vikoba hivyo kwa kupitia ushirikiano huu wateja wa benki yetu wataweza kuzifikia akaunti kirahisi mahali walipo na kwa wakati wowote na kupata huduma.
Alisema kwa kupitia DCB VicobaApp, wateja wa vicoba wataweza kupata huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka pesa bila makato yoyote, kukopa mikopo na kufanya marejesho, kuchagua viongozi wa wa vikundi vyao, kupata ujumbe mfupi kwa kila mjumbe pale mjumbe mmoja anapoweka pesa kwenye kikoba, yote yakifanyika kupitia simu za mkononi.
Naye Mkurugenzi wa Biashara wa DCB, Bi. Lilian Mtali alisema benki yao inajivunia kuwa moja ya benki waanzilishi kwa kutoa mikopo ya wajasiriamali ikiwemo mikopo midogomidogo ya kuanzia hata kiasi cha shs elfu 30 hadi milioni 5 kwa wateja wadogo.
"DCB pia tunajivunia kutoa mikopo ya kiasi cha shs trilioni 1 kwa wajasiriamali na wafanyakazi ambapo sasa benki inao uwezo wa kutoa mkopo wa hadi kiasi cha shs bilioni 5 kwa mtu mmoja.
“Katika kuhakikisha lengo letu la kuboresha maisha ya watanzania na kuwapunguzia umasikini linatimia, DCB kila mara imekuwa ikianzisha akaunti na huduma zenye ubunifu, mfano akaunti ya elimu ya DCB Skonga, Wahi Akaunti kwa wenye mahitaji ya kutimiza malengo kwa njia ya kuwekeza kidogo kidogo, akaunti za Mshahara & Mikopo ya nusu mshahara, akaunti ya Wastaafu, Mikopo ya Nyumba, Akaunti maalum (FDR) na nyinginezo nyingi,” aliongeza Bi Lilian.
Ikiwekeza zaidi katika huduma za kibenki kwa njia za kidigitali, DCB ina mtandao wa mawakala zaidi ya 1500 na vituo vidogo vya kutokea huduma zaidi ya 700 katika maeneo ya kimkakati sehemu mbalimbali nchini huku ikiwa na mtandao wa Matawi 9 ya kibenki jijini Dar es Salaam na mikoani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara DCB, Bwana Sabasaba Moshingi (katikati), Mkurugenzi wa Biashara wa benki hiyo, Bi. Lilian Mtali (kulia) na Mkurugenzi wa Shirikisho la Vikundi vya Ujasiriamali Tanzania (SHIVUTA), Andrew Paul wakiwasili tayari kwa uzinduzi programu ya DCB Vicoba pamoja na uzinduzi wa mradi wa kumiliki Coaster 5 wa Umoja wa Vikundi vya Ujasiriamali Kivule (UVUKI) uliopo chini ya Shirikisho la Vikundi vya Ujasiriamali Tanzania (SHIVUTA) uliofanyika Kitunda, Ilala, jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya Wana vikoba waliohudhuria uzinduzi wa DCB VikobaApp wakiwa katika hafla hiyo, Kitunda, Ilala, Dar es Salaam leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara DCB, Bwana Sabasaba Moshingi (katikati) akiagana na Mkurugenzi wa Shirikisho la Vikundi vya Ujasiriamali Tanzania (SHIVUTA), Bwana Andrew Paul mara baada ya uzinduzi programu ya DCB Vicoba pamoja na mradi wa kumiliki Coaster 5 wa Umoja wa Vikundi vya Ujasiriamali Kivule (UVUKI) uliopo chini ya Shirikisho la Vikundi vya Ujasiriamali Tanzania (SHIVUTA) uliofanyika Kitunda, Ilala jijini Dar es Salaam leo. Wengine ni Viongozi wa Umoja wa Vikundi vya Ujasiriamali Kivule (UVUKI).
No comments