Breaking News

MY LEGACY WAFANYA USAFI SOKO LA KAWE

 Na Mwandishi Wetu 

Shirika lisilo la Kiserikali la My Legacy ambalo dhumuni na lengo lake kubwa ni kujaribu kupunguza umaskini uliokithiri kwenye jamii kupitia kuwezesha makundi mbalimbali kama vile wanawake na Vijana ambapo limeshatekeleza miradi mbalimbali kwa mafanikio makubwa ikiwemo ule Mradi maarufu wa WASH , Leo Desemba 02, 2023 limeshiriki zoezi la kufanya usafi katika soko la Kawe kwa lengo la kuhamasisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kujijengea tabia ya kufanya usafi wa mazingira kwa vitendo bila kusubiri kusukumwa na serikali .

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya zoezi hilo la usafi katika maeneo mbalimbali ya soko la Kawe Afisa Miradi kutoka shirika hilo Bw. Julius Prinsipatus amesema kuwa shirika la My Legacy linaamini kwamba suala la usafi na utunzaji mazingira ni la wanajamii kwa maana athari zozote zinazotokana na uchafuzi wa mazingira linaifikia jamii moja kwa moja kwahiyo wananchi inabidi wawe msitari wa mbele kusafisha na kutunza mazingira bila kusubiri kusukumwa na serikali.

"Tupo hapa  tunahamasisha wanajamii na Uongozi wa sehemu hii kujitolea kufanya usafi na kutunza mazingira ili kuweza kupunguza matatizo mbalimbali yanayotokana na uchafu, tumeshafanya hivi katika maeneo mbalimbali ikiwemo soko la Kunduchi ambapo tulipanda na kuhamasisha upandaji wa miti, Ombi langu kwa serikali ni kwamba tunaiomba iweze kutuunga mkono wadau kama sisi ambao tunajitolea kuhamasisha wanajamii, lakini waweze kuangaliaa sehemu mbalimbali zenye changamoto za uchafuzi wa mazingira na kuzitatua". Amesema Bw. Julius
 
Nao kwa nyakati tofauti tofauti Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa Mzimuni Bi. Raiya Nassor, Mwenyekiti wa Soko la Kawe Bw. Yusuph Abdallah, na Mfanyabiashara Omary Mohammed wamelipongeza Shirika la My Legacy kwa kuhamasisha suala la usafi na Utunzaji wa Mazingira katika maeneo mbalimbali Nchini, lakini pia uanzishaji wa Miradi mbalimbali yenye lengo la kuleta mabadiliko chanya katika jamii ya Tanzania

No comments