Breaking News

MWANAHARAKATI BIHIMBA MPAYA ACHANGIA TOFALI 500 UJENZI WA UZIO ABUJUMAA SEKONDARI

.

Mwanaharakati Bihimba Mpaya ( Kulia ) akisalimiana na wazazi pamoja na walimu  kwa kuwapungia mkono baada ya kukabidhi msaada wa tofali 500 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Uzio katika Sherehe za Mahafali ya Kidato cha nne Shule ya Sekondari ABUJUMAA iliyoko Ilala Jijini Dar Es Salaam , Oktoba 19 , 2023.


Mwanaharakati Bihimba Mpaya akiongoza Harambee ya wazazi kuchangia Ujenzi wa Uzio katika Sherehe za Mahafali ya Kidato cha nne Shule ya Sekondari ABUJUMAA iliyoko Ilala Jijini Dar Es Salaam , Oktoba 19 , 2023.


Tofali 500 zenye thamani ya Shilingi Laki Tano alizotoa Bihimba kwa ajili ya Ujenzi wa Uzio Abuyjumaa Sekondari

Bihimba Mpaya akiburudika kwa kucheza mziki na wahitimu wa kidato cha nne katika Sherehe za Mahafali yao Shule ya Sekondari ABUJUMAA iliyoko Ilala Jijini Dar Es Salaam , Oktoba 19 , 2023.
                                                              Na Regina Mkonde .

MWANAHARAKATI huru, Bihimba Nasoro Mpaya, amesaidia ujenzi wa ukuta wa shule ya Sekondari ya Abbuy Jumaa, iliyoko Kivule jijini Dar es Salaam, kwa kuipatia matofali 500 yenye thamani ya Sh. 500,000, pamoja na mifuko ya saruji 20.

Bihimba amekabidhi vifaa hivyo vya ujenzi leo tarehe 19 Oktoba 2023, katika mahafali ya 14 ya wanafunzi wa kidato cha nne, yaliyofanyika shuleni hapo baada ya Mkuu wake wa shule, Froida Nkya, kuwaomba wadau watoe misaada itakayosaidia kutatua changamoto zinazoikabili.

Mwanaharakati huyo amesema kuwa, ameamua kutoa mchango huo ili kusaidia kuboresha mazingira mazuri ya shule, yatakayowasaidia watoto kusoma vizuri pamoja na walimu wake kufanya kazi kwa moyo.

                          

“Hii si mara ya kwanza kuisaidia shule hii, hadi sasa nimeshatoa mifuko 20 ya saruji pamoja na matofali 500, kwa ajili ya ujenzi wa ukuta ambao umekwama, naamini ukuta huu ukimalizika changamoto za watoto kutoroka na hata ukosefu wa ulinzi na usalama shuleni itapungua,” amesema Bihimba na kuongeza:

“Hii shule ni ya kata , wenye mamlaka ni wananchi ambao ni wazazi wenye watoto wanaosoma pale hivyo inapaswa kujengwa kwa nguvu zao. Kweli serikali ipo lakini wananchi tunapaswa kusaidia vitu vidogovidogo.”

Mbali na Bihimba, wananchi mbalimbali walifanya harambee kwa ajili ya kuchangisha fedha za ujenzi wa ukuta, ambapo zilipatikana zaidi ya Sh. 400,000, huku wengine wakiahidi kutoa matofali na vifaa vingine.

                           

Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Dkt. Katanta Simwanza, aliahidi kutoa kompyuta tatu, kuunganisha Shule hiyo na huduma ya intaneti, pamoja na kuwatafuta wadau wengine zaidi kwa ajili ya kuisaidia shule hiyo.

Awali, Nkya aliwaomba wadau watoe michango yao ya hali na mali kwa ajili ya kutatua changamoto hizo, ikiwemo uhaba wa matundu ya vyoo 50 ambapo kwa sasa viko 14 na vinavyohitajika ni 64. Chumba cha wanafunzi na walimu wa kike kujihifadhi wakiwa katika siku za hedhi na vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hususan kompyuta.

“Tunamshukuru Bihimba kwa kutoa msaada huu ambao utatusogeza kidogo kwenye ujenzi wa ukuta, lakini bado tunahitaji misaada mingine,” amesema Nkya.

                       

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya Abuuy Jumaa, Emanuel  Kimaro, amesema shule hiyo inakwamba kutatua changamoto ndogondogo kutokana na wazazi na walezi wa wanafunzi kuwa wazito kutoa michango itakayowezesha kuitatua.

                       

No comments