Breaking News

DIT YAWANOA WALIMU WA SEKONDARI KATIKA TEHAMA HUSUSAN MATUMIZI YA VISHIKWAMBI , PROF. MDOE APONGEZA ( + VIDEO )

 Na Mwandishi Wetu


TAASISI ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imeanza kutoa mafunzo kwa walimu waliopatiwa vishkwambi baada ya kubaini baadhi yao wakiwaachia watoto wachezee badala ya kuvitumia kufundishia.


Aidha, imesema walimu hao pia wanapaswa kufundishwa namna ya kutengeneza vishkwambi hivyo pindi vitakapoharibika ili kuwe na matumizi endelevu badala ya kuvitelekeza.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kituo cha Umahiri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa DIT, Dk Petro Pesha alisema lengo la serikali kugawa vishikwambi hivyo ni kuboresha mazingira ya ufundishaji na kuhamasisha matumizi ya teknolojia.

Alisema kuwa ili kuwe na matumizi endelevu ya vishkwambi hivyo, walimu wanapaswa kuvilinda na kuvitunza ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

"Tuliona mahitaji makubwa kwa walimu waliopewa vishkwambi hivi hawajui jinsi ya kuvitumia wala kuvitengeneza pale vinapoharibika hivyo huwaachia watoto wao wachezee," alisema Dk Pesha.

Aliongeza kuwa vishkwambi vikitumika ipasavyo vitawezesha utoaji wa elimu bora hivyo ni muhimu kuvitengeneza ili isiwe mwisho wa matumizi.

Dk Pesha alisema vishkwambi vinaweza kutumika kufundishia, kuwasilisha taarifa za kufundishia, kutafuta taarifa mtandaoni na kuchakata taarifa na matokeo ya wanafunzi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe alisema lengo la kutolewa kwa vishkwambi hivyo ni kuboresha utoaji wa elimu nchini na kuwarahisishia kazi walimu.

Alisema katika mapinduzi ya nne ya viwanda, ni lazima walimu waendelee kujifunza masuala mbalimbali ya Tehama ili kupata maarifa yatakayowasaidia katika kazi zao.

"Serikali imetaka kurahisisha kazi zenu kwani kwa kutumia vishkwambi mnaweza kupata reference za vitabu mbalimbali mkavipakua mtandaoni na kufundishia...mkubali kubadilika muende na wakati na msiache kujifunza masuala ya teknolojia, mtapoteza maarifa," alisisitiza Profesa Mdoe.

Kwa upande wake, Mkuu wa DIT, Profesa Preksedis Ndomba alisema mafunzo hayo yameanza kutolewa katika Kampasi za Dar es Salaam na Mwanza kuanzia Juni 12 hadi 22, mwaka huu.

Alisema wameanza kutoa mafunzo kwa walimu 33 wa Shule za Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Temeke na wengine 200 wa mkoani Mwanza.

"Tuko tayari kutoa mafunzo katika Kampasi zote tatu ikiwemo Songwe kwani tunahitaji walimu wafahamu matumizi sahihi ya vishkwambi kwa kutimiza malengo yaliyokusudiwa," alisema.

Naye, Mwalimu Asteria Kimambo alisema wamejifunza kutumia programu za ofisi, kuandaa na kutathmini mitihani, ripoti na barua za wito kwa wazazi.

Hata hivyo, aliomba wawezeshwe kikamilifu ili kuhudhuria mafunzo wanayotakiwa ipasavyo sambamba na kuongezwa kwa muda wa mafunzo.

No comments