BARAZA LA TAASISI YA TEKNOLOJIA DAR ES SALAAM ( DIT ) LAZINDULIWA NA KUPEWA MAJUKUMU MAZITO
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda leo amezindua Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na kuliagiza kuimarisha ushirikiano na Taasisi na Kampuni kubwa duniani na pia kubiasharisha bunifu zinazozalishwa ndani ya Taasisi hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi wa Baraza hilo, Prof. Mkenda amelitaka Baraza hilo kuongeza ushirikiano na Kampuni ili kupata utaalamu kutoka Taasisi hizo kubwa sambamba na kukuza ujuzi kwa wataalam wa ndani.
"Sisemi kwamba hamfanyi, hapana katika hili naomba niwapongeze sana DIT lakini nilitake Baraza hili liongeze ushirikiano na Taasisi hizo na hasa Taasisi za China ambako kuna ujuzi mkubwa"
"Niwaambie tu kwamba mmeshikilia fursa za ajira za watanzania kwenda nje kujifunza na kuja nchini kushika ajira....... au mlete wataalam kutoka huko kuja kufundisha hapa kwetu watuachie utaalam wao," amesema Prof Mkenda.
Prof. Mkenda amesema moja ya changamoto iliyopo ni kampuni mbalimbali za nje ya Tanzania zinakuja nchini lakini zinakosa wataalam kushika ajira katika kampuni zao, ameelekeza pia Baraza hilo kusimamia mafunzo ambayo yanaendana na hitaji la viwanda.
Ameagiza pia, kutazama fursa zilizopo katika miradi mikubwa ya kimkakati akitolea mfano Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, Bomba la Mafuta la Uganda na Treni ya kwenda haraka, kuanzisha mafunzo ambayo yatazalisha wataalam wa kuendesha miradi hiyo.
"Tujenge mfumo wa kujua uhitaji je ni wataalam wa aina gani wanahitajika, ili tufanye mafunzo kuendana na mahitaji hayo hata ikiwezekana kuagiza wataalam kutoka nje kufundisha, au kupeleka wataalam wetu kupata ujizi na kuja kufundisha au kuanzisha kozi fupifupi, tunachotaka sisi ni watu wetu wapate hizo ajira," amesema Prof. Mkenda.
Ameagiza pia Baraza baada ya ziara katika Kampasi za Taasisi hiyo, kupata nafasi ya kuzungumza na watumishi pamoja na wanafunzi kujua changamoto zao na hasa katika vitendea kazi ikiwa ni pamoja na mashine za kisasa za kufundishia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo, Dkt. Richard Masika ameahidi Baraza lake kupokea maelekezo hayo na kufanyia kazi kwa haraka. Amesema, "tukuahidi tu kwamba maelekezo hayo tumeyapokea na kuanza kufanyia kazi mara moja, tutakua tukitoa mrejesho mara kwa mara."
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya ElimuSayansinaTeknolojia, Prof James Mdoe amesema ana imani kubwa na wajumbe wa Baraza hilo kutokana na weledi pamoja na taaluma zao. Ameongezakuwa DIT inatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika elimu ya amali.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la DIT, Mwema Punzi akitoa neno la shukrani ameahidi kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi mkubwa kwa kutumia taaluma zao.
No comments