Breaking News

Benki ya DCB yazidi kujiimarisha kimtaji na kuendelea kupata faida

      
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Biashara ya DCB, Alexander Sanga (wa tatu kushoto) akiwa na baadhi ya wajumbe wa bodi ya benki hiyo wakati wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Mwaka wa Wanahisa wa benki hiyo 2023 jijini Dar es Salaam jana. Kutoka kushoto ni Mwanasheria wa benki hiyo, Alex Mgongolwa, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Isidori Msaki na wajumbe wengine; Dk. Amina Baamary, Cliff Maregeli na David Shambwe.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Biashara ya DCB, Alexander Sanga akifungua Mkutano Mkuu wa 21 wa Mwaka wa Wanahisa wa benki hiyo jijini Dar es Salaam jana
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Isidori Msaki akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Mwaka wa Wanahisa wa benki hiyo jijini Dar es Salaam jana
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Biashara ya DCB, Dk. Amina Baamary (kulia) akizungumza na baadhi ya wanahisa na wajumbe wengine wa bodi hiyo, baada ya kumaliza Mkutano Mkuu wa 21 wa Mwaka wa Wanahisa wa benki hiyo jijini Dar es Salaam Jana.
Sehemu ya wanahisa wa Benki ya DCB wakihudhuria Mkutano Mkuu wa 21 wa Mwaka wa Wanahisa wa benki hiyo, jijini Dar es Salaam jana.

Na Mwandishi Wetu,

BENKI ya Biashara ya DCB imeendelea kujivunia kuongezeka kwa mtaji wake huku ikijiendesha kwa faida inayoongezeka kila mwaka licha ya changamoto kadhaa za kiuchumi, wanahisa wa benki hiyo wameelezwa jijini Dar es Salaam jana

Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Mwaka wa Wanahisa wa DCB, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Bi. Zawadia Nanyaro alisema benki yao ipo imara kimtaji unaofikia kiasi cha shs 28.5 bilioni unaovuka vigezo vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) vya shs 15 bilioni vilivyowekwa kwa benki za biashara.

Benki yetu ilipata faida baada ya kodi ya shs 747 milioni kwa mwaka 2022, faida iliyochangiwa na mapato yasiyotokana riba ya shs 10.3 bilioni ambayo ni mafanikio ya asilimia 111 ya malengo tuliyojiwekea kwa mwaka 2022, huku mapato yatokanayo na riba yakifika shs 28.6 bilioni ikiwa ni asilimia 86 ya malengo tuliyojiwekea".

Mazingira ya uendeshaji wa taasisi za fedha kwa mwaka 2022 yaliendelea kuwa tulivu huku thamani ya shilingi ya kitanzania ikiendelea kuimarika dhidi ya mataifa mengine, uchumi ukikua tena baada ya janga la Uviko-19, mfumuko wa bei ukiendelea kuwa chini kwa mwaka mzima, mafanikio katika sekta ya utalii na kufunguliwa kwa milango ya biashara kumechagiza kwa DCB kuendelea kufanya vizuri sokoni”,

Akizungumzia utendaji wa benki, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa wa benki hiyo Bw. Isidori Msaki alisema DCB imekuwa makini katika kusimamia mikakati yake ya muda mrefu jambo linaloleta matokeo chanya ikiwemo kukua kwa mali za benki.

Mwaka 2022 mali za benki zimekuwa hadi kufikia shs 211 bilioni kutoka shs 192 bilioni kwa mkwa 2021, ukuaji ulioitoa benki yetu kutoka kwenye kundi la benki ndogo za biashara hadi kufikia benki za kati nchini."

DCB imeendelea kulinda thamani ya wanahisa wake kwa kukuza mapato yasiyotokana na riba kutoka asilimia 30 ya mapato yote mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 49 kwa mwaka 2022 ongezeko lililotokana na kuimarika kwa mifumo ya kidigitali inayochangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la miamala kwa zaidi ya asilimia 135”, alisema Bwana Msaki.

Akizungumzia baadhi ya vipaumbele vya benki hadi ifikapo mwaka 2025 kwa wanahisa waliofurika katika ukumbi wa JK Nyerere International Conference Centre jijini humo mkurugenzi huyo alisema ni kuhakikisha huduma za benki hiyo zinapatikana nchi nzima na hiyo inawezekana kwa kupitia hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma zake kwa njia za kidigitali.

Tumeanzisha vituo vidogo vya huduma katika maeneo ya kimkakati, huduma za mawakala zaidi ya 700 nchini kote pamoja na mtandao wa matawi saba ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam".

Benki yetu inalenga kuongeza wigo wa kutoa mikopo kwa njia za kidigitali kwa kiwango kikubwa ifikapo mwaka 2025, mwaka 2022 tulitoa mikopo isiyopungua shs 1.2 bilioni, mikopo hii ni salama zaidi kwa sababu inalipwa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja” , aliongeza mkurugenzi huyo.

Aidha mkurugenzi huyo alisema DCB inaendelea na mkakati wake wa kuhakikisha inapata faida mwaka hadi mwaka ili kufikia thamani ya hisa ya asilimia 18.9 na kuendelea kupunguza uwiano wa mikopo chechefu hadi kufikia chini ya asilimia 5 na pia kuongeza idadi ya wateja.

Aliwaomba wanahisa hao kuzidi kuwekeza ndani ya benki yao na kuzidi kuiamini menejimenti na bodi kwani uwekezaji wao umeleta faida kubwa kwa maisha ya watoto wa watanzania kwani umewawezesha kutoa msaada wa madawati kwa shule zenye uhitaji mkubwa jambo linalowapa amani watoto hao kusoma katika mazingira bora.

Ni kwa uwekezaji wenu wanahisa wetu uliotuwezesha pia kutoa elimu ya ujasiriamali kwa watanzania, elimu hii ni muhimu katika maendeleo ya biashara na maisha yao, tutaendelea kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi wetu ili kuendelea kuleta matokeo chanya”, alisema.

Pamoja na kupata faida ya baada ya kodi ya sh 747 milioni 2022, na kwa kuzingatia sheria ya Benki Kuu, Bodi ya Wakurugenzi ya DCB imependekeza faida iliyopatikana ikaongeze fedha za wanahisa badala ya kutoa gawio.

No comments