Msaidizi wa kisheria amsaidia mtoto aliyetelekezwa na mama yake
Kumekuwa na ripoti juu ya baadhi ya wazazi kuwatelekeza watoto wao na kuwafanya wakose haki zao za msingi kinyume cha sheria.
Wakati kifungu cha 7 cha Sheria ya Mtoto (2009) kinatoa haki ya mtoto kukua akiwa na wazazi wake, kifungu cha 8 kinatoa wajibu kwa mzazi, mlezi au mtu yeyote anayemtunza mtoto na hasa wajibu huu unampa mtoto haki ya kupata chakula, malazi, mavazi, huduma ya afya, ikiwa ni pamoja na kupata chanjo, elimu na mwongozo, uhuru na haki ya kucheza na kupumzika. Hata hivyo, yote haya hayafanyiki kwa baadhi ya familia nchini.
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka miwili, Victoria Dotto, aliyezaliwa Wilaya ya Malinyi alitelekezwa hivi karibuni na mama yake Joyce Ishengela na haijulikani mahali mama huyo alipo na hakuna anayejua sababu zilizomfanya amtelekeze mtoto wake.
Bi Ishengela, ambaye pia ametelekezwa na mume wake kwa muda sasa, alizaliwa Mkoa wa Mwanza mwaka 2002. Alienda kwa dada yake Bi Mbuke Madini Wilaya ya Malinyi akiwa na mtoto wake, ambaye alimtelekeza baadaye.
Mpita njia mmoja, Bw Ally Mkutila, alimkuta mtoto huyo akiwa peke yake alipokuwa akienda kulima shambani kwake. Njia aliyopita ilikuwa karibu na nyumba ya Bi Madini, ambapo mtoto huyo aliachwa bila ya kuwa na mwangalizi yeyote.
Bw Mkutila alishangaa kwa nini mama amwache mtoto wake katika mazingira kama yale na hivyo alimjulisha msaidizi wa kisheria baada ya kuona mtoto yuko kwenye mazingira yasiyo rafiki na salama kwa mtoto.
Baada ya Bw Mkutila kutoa habaria Kituo cha Wasaidizi wa Kisheria Malinyi, mmoja wa wasaidizi wa kisheria alienda kumwona mtoto huyo na kumkuta katika mazingira ya hatari.
“Nilimkuta mtoto kwenye mazingira hatarishi. Hapakuwa na mtu wa kumsaidia mtoto nilipofika nyumbani hapo. Niliuliza mahali alipo mama yake na hakuna mtu aliyejua alipoenda,” alisema msaidizi wa kisheria Bi Martha Elimba, aliyeamua kumchukua mtoto huyo hadi kituoni kwao. “Mtoto alikuwa bado mchanga kuachwa katika mazingira yale peke yake.” Bi Elimba alitoa taarifa Ofisi ya Ustawi wa Jamii wilayani kwa hatua zaidi.
Kituo cha Wasaidizi wa Kisheria Malinyi, kwa ushirikiano na Ofisi ya Ustawi wa Jamii Wilaya ya Malinyi, kilimjulisha Mkurugenzi wa Wilaya ya Malinyi Bw Musa Mnyeti juu ya mtoto aliyetelekezwa na mkurugenzi akatoa kiasi cha shilingi 180,000 kwa ajili ya kusaidia matunzo ya mtoto. Baadaye mtoto huyo alipelekwa Hospitali ya Lugala ya Kanisa la Kilutheri Wilaya ya Malinyi. Ofisi ya Ustawi wa Jamii iliandika barua ya utambulisho kwa wasaidizi wa kisheria ili kurahisisha mapokezi ya mtoto.
Daktari wa hospitali hiyo Emmanuel Chogo alimpokea mtoto na baada ya uchunguzi alishauri mtoto alazwe na kubaki hospitalini hapo hadi atakapofikisha uzito wa kilo 9 kwani alionekana kuwa na uzito chini ya wastani kwa sababu ya ukosefu wa lishe bora.
Habari zinasema, motto huyo sasa hivi anaendelea vizuri, asante kwa msaada na ushirikiano ulifanywa na msamaria wema, wasaidizi wa kisheria, mkurugenzi wa wilaya, daktari wa hospital ya Lugala, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, na wote walihusika kumsaidia motto huyo.
No comments