Benki ya Biashara ya DCB yaingia kwenye mizania ya kati na yajiimarisha kwa kuendelea kupata faida zaidi mwaka 2022 huku amana na mali zikiongezeka
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB , Bwana Isidori Msaki
DAR ES SALAAM, Januari 31, 2023. Benki ya Biashara ya DCB imepata faida kwa kiwango kikubwa kwa mwaka wa fedha wa 2022 ukilinganisha na faida iliyopatikana kwa kipindi kama hicho mwaka 2021 huku mali za benki hiyo na amana zikiongezeka.
Katika mwaka wa fedha wa 2022, benki ya DCB ilijipatia Faida Kabla ya Kodi ya shilingi za Kitanzania 2.25 bilioni, ikilinganishwa na faida ya shilingi 1.06 bilioni kwa mwaka wa fedha 2021, ikiwa ni kukua kwa faida kwa asilimia 112.
Ukuaji huu unatokana na kuongezeka kwa kwa mapato ya benki kwa asilimia 11, ambapo ulisababishwa na ukuaji wa mapato yatokanayo na riba ambayo yaliongezeka kwa asilimia 4 hadi kufikia shilingi 28.61 bilioni, ikilinganishwa na shilingi 27.62 bilioni mwaka 2021, na mapato yasiyotokana na riba ambayo yaliongezeka kwa asilimia 45 kutoka shilingi 7.2 bilioni hadi shilingi 10.4 bilioni kati ya mwaka 2021 na 2022 kwa pamoja.
“Benki ilifanikiwa kukuza mapato katika mwaka wa fedha ikijiita katika shughuli za utoaji wa mikopo kwenye shughuli za biashara, biashara ya fedha za kigeni, na ongezeko la ada ya miamala kutokana na maboresho ya vitengo mbalimbali vya huduma na ongezeko la matumizi ya huduma za kibenki kidigitali,” alisema Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa DCB , Bwana Siriaki Surumbu.
Benki vilevile iliimarisha nafasi yake kama benki ya ukubwa wa kati yenye mizania ya shilingi bilioni 200, mali zake zikifikia thamani ya shilingi bilioni 214 kwa mwaka 2022. Huu ni ukuaji wa asilimia 61 kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2018 ambapo thamani ya mali za benki ilikuwa ni shilingi billion 133.
Jengo la Makao Makuu ya Benki ya DCB, Magomeni, jijini Dar es Salaam
Jumla ya mikopo mwishoni mwa mwaka 2022 ilikuwa ni shilingi 130.36 bilioni, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 4 ukilinganisha na shilingi 125 bilioni mwaka 2021. Uwekezaji wa benki katika dhamana za serikali uliongezeka kwa asilimia 44 hadi kufikia shilingi 41 bilioni kutoka shilingi 28 bilioni mwaka 2021. Amana za benki ziliongezeka kwa asilimia 11 kutoka shilingi 150 bilioni mwaka 2021 hadi kufikia shilingi 165 bilioni mwaka 2022, ongezeko hilo lilitokana na mikakati mahsusi ya benki ya kuongeza wigo wa huduma za fedha kwa wateja wake.
“Katika mwaka huo benki ilisherehekea tuzo kadhaa na kuibuka kinara katika Tuzo za ‘Consumer Choice Africa Award’ (CCAA), ikiibuka mshindi katika kitengo cha benki inayopendwa zaidi katika huduma kwa wateja Tanzania. Benki vilevile ilishinda tuzo ya uwasilishaji wa taarifa bora za fedha inayotolewa na NBAA, katika kundi la benki za ukubwa wa kati, ikishikilia ushindi wa miaka mitano mfululizo katika tuzo hiyo,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Bwana Isidori Msaki.
Tuzo hizo zilikuwa ni faraja kubwa kwetu na kwa wadau wetu wote, ikizingatiwa kuwa DCB ilikuwa ikisherehekea miaka 20 ya kuendesha biashara kufikia mwishoni mwa mwaka 2022. DCB inaendelea kusherehekea ubora wa viwango vyake huku ikitazamia utendaji bora zaidi kwa mwaka 2023.
No comments