Breaking News

BATIKI YA TANZANIA SASA KUWEKEWA VIWANGO NA TBS

 

Na Mwandishi Wetu- DSM

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema katika stadi za ujasiriamali Vazi la Batiki litawekewa viwango ili mtu yeyote Duniani akishika vazi letu itambulike kuwa ni Batiki kutoka Tanzania.

Waziri Dkt. Gwajima ametoa kauli hiyo leo Julai 08, 2022 wakati wa Siku ya vazi la Batiki ambayo imefanyika kwenye Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam wakati wa Maonesho ya 46 ya Biashara yanayoendelea.

“Tunataka mahali popote vazi hili la Batiki mtu akilishika ijulikane kuwa ni Batiki ya Tanzania kwani ni kwa njia hiyo tutaweza kuwakomboa watu wetu na Umasikini” amesema Dkt. Gwajima.

Ameongeza kwamba, lengo ni kuwafikia watengenezaji wa Batiki wakiwemo Wanawake walio wengi kwenye Sekta ya Biashara ndogo ndogo ili kila mmoja aweze kuinuka kiuchumi.

This image has an empty alt attribute; its file name is 8644cf71-949f-40cb-b181-f7228a0c9556-1024x683.jpg

Dkt. Gwajima amesema kuwa, Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amefungua fursa kwa Wanawake na kuwaonesha kuwa wanaweza, hivyo nimuhimu kuchapa kazi kwa kushirikiana na Wanaume kuinua Uchumi wa Nchi.

“Kutungwa kwa Sheria ya Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka 2018 inayozitaka Halmashauri zote kutenga 10% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa makundi maalum ikiwemo wanawake imewasaidia wengi ambapoMwaka 2020/21 zilitengwa jumla ya Sh. Bil. 62.68 na kufikia 30th Juni, 2021 Sh. Bil. 53.81 zilikopeshwa kwa Vikundi 7,993 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu sawa na asilimia 86” alisema Dkt. Gwajima.

Amebainisha kuwa, kati ya Fedha hizo Sh. Bil. 28.17 zilitolewa kwa vikundi vya wanawake 4,894 vilivyozalisha ajira 52,428.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe amewahimiza waandaaji wa Siku ya Batiki kufanyika nchi nzima.

This image has an empty alt attribute; its file name is 6f29379f-2418-4c17-b8ea-4d1a9f28ad9f-1024x683.jpg

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Zainab Chaula ameahidi kushirikiana na Katibu Mkuu wa Zanzibar kufanyia kazi maelekezo ya Mawaziri hao.

Awali Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara TanzaniaBi. Latifa Mohamed Khamis, aliomba Serikali kuhakikisha Shirika la Viwango nchini TBS, wanatoa Vyeti vya Ubora wa Bidhaa za Batiki.

No comments