YAS WAWASAIDIA WENYE MATATIZO YA MACHO BURE SABA SABA
Na Adery Masta.
Katika kuadhimisha Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam—maarufu kama Sabasaba—kampuni ya mawasiliano ya Yas kwa kushirikiana na Taasisi ya Bilal Muslim na Khoja Shia Ithnaseri Charitable Eye Centre imeendesha zoezi maalum la upimaji wa macho na kutoa miwani bure, likilenga kuwahudumia Watanzania kwa njia ya kipekee na yenye kugusa maisha.
Zoezi hilo linalofanyika kwa siku tatu mfululizo, limepangwa kuwafikia zaidi ya watu 600, huku likiwa ni sehemu ya kampeni kubwa zaidi inayolenga kuwahudumia takribani watu 16,000 nchi nzima katika kipindi cha muda, na huku likitarajiwa kutamatishwa Leo Jumamosi ya Julai 5, 2025 saa Tisa na nusu Alfajiri.
Kwa mujibu wa tafiti, asilimia 20 ya Watanzania wanakabiliwa na changamoto za afya ya macho, hali inayoathiri kwa kiasi kikubwa ubora wa maisha, uwezo wa kufanya kazi na kujifunza. Kwa kulitambua hilo, Yas imeamua kutumia jukwaa la Sabasaba kuleta huduma hii karibu zaidi na wananchi.
Akizungumza katika banda lao, Daktari wa macho kutoka Taasisi ya Bilal, Ain Sharif, ameipongeza Yas kwa uamuzi wa kuwekeza kwenye afya ya jamii.
"Tunaishukuru Yas kwa kutambua umuhimu wa macho kwa maisha ya kila siku. Huduma hii si tu inawasaidia watu kugundua matatizo ya macho mapema, bali pia inawapatia suluhisho la haraka," alisema Dkt. Sharif.Kwa upande wa Yas, Meneja wa Mahusiano ya Nje, Rukia Mtingwa, amesema kuwa zoezi hili ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo katika kurudisha kwa jamii:
> "Kupitia Sabasaba, tumepata fursa ya kuwafikia Watanzania kwa karibu zaidi. Hii ni sehemu ya mpango mpana wa huduma kwa jamii tunaoendelea nao nchini kote."
Wananchi waliopata huduma hii wameonyesha furaha na shukrani kwa Yas na Taasisi ya Bilal. Wengi wao wamesema kuwa huduma hiyo imekuwa mkombozi, hasa kwa wale ambao hawakuwa na uwezo wa kulipia vipimo na miwani.
“Nilijua macho yangu yanashida, lakini sikuweza kwenda hospitali kwa sababu ya gharama. Leo nimepimwa na nimepewa miwani na sawa bure. Nashukuru sana Yas,” alisema mmoja wa wananchi waliohudhuria zoezi hilo.
Kwa kuchukua hatua kama hizi, Yas inaonesha mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na taasisi za kijamii katika kuboresha maisha ya Watanzania. Huduma hii ya upimaji wa macho bure inakuwa si tu msaada wa kiafya, bali pia ni dira ya kujali na kujenga jamii yenye kuona vyema—kwa maana ya macho na hata matarajio ya maisha bora.
No comments