YAS TANZANIA YAZINDUA ‘SGR YAS STORE’ KATIKA STESHENI YA SGR DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam, Machi 19, 2025 – Yas Tanzania imezindua rasmi duka lake jipya, SGR Yas Store, katika Stesheni ya Reli ya Kisasa (SGR) jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua muhimu ya kusogeza huduma zake karibu zaidi na wateja. Uzinduzi huu unafanyika sambamba na maadhimisho ya siku 100 tangu kubadilishwa rasmi kwa chapa za Tigo na Tigo Pesa kuwa Yas na Mixx by Yas.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bi. Flora Mgonja, Afisa Tawala Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema, "Uzinduzi wa SGR Yas Store ni hatua muhimu katika kuboresha huduma kwa abiria wa SGR kwa kuhakikisha wanapata huduma za kidijitali na kifedha kwa urahisi zaidi. Naipongeza Yas kwa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa hasa kwenye spidi ya Intaneti. Sisi kama Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam tupo tayari kuwapa ushirikiano ili mfanye kazi zenu kwa ufanisi zaidi”.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Mixx by Yas, Bi. Angelica Pesha, alieleza kuwa SGR Yas Store ni sehemu ya mkakati wa kampuni wa kuwaunganisha Watanzania na huduma za kidijitali kwa urahisi zaidi.
"Uzinduzi wa duka hili ni hatua muhimu kwa Yas na Mixx, tukidhamiria kuhakikisha upatikanaji rahisi wa huduma za mawasiliano na kifedha kwa wateja wetu. Wateja sasa wanaweza kupata huduma zote muhimu ikiwemo kusajili laini, kufanya malipo kupitia Mixx, na hata kukata tiketi za SGR moja kwa moja kupitia mini-App ya TRC iliyo ndani ya Super App ya Mixx by Yas," alisema Bi. Pesha.
Kwa mujibu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), wastani wa abiria 300,000 husafiri kwa SGR kila mwezi, hivyo kuwepo kwa SGR Yas Store katika kituo kikuu cha Dar es Salaam ni fursa muhimu ya kuboresha huduma kwa abiria.
Katika kuimarisha ushirikiano wake na TRC, Yas imezindua ofa maalum kwa wateja wa Mixx, ambapo kila Ijumaa, wateja watakaonunua tiketi za SGR kwa kutumia Mixx by Yas watarudishiwa asilimia 100 ya gharama ya nauli yao.
Licha ya uzinduzi huu, Yas Tanzania inaendelea na mpango wa kupanua mtandao wake wa maduka, ambapo ifikapo mwisho wa mwaka huu, kampuni inatarajia kuwa na zaidi ya Yas Store 80 na Yas Express 300 katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa hatua hii, Yas Tanzania inaendelea kuimarisha nafasi yake kama mshirika wa kuaminika katika sekta ya mawasiliano na huduma za kifedha za kidijitali, huku ikichochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Post Comment
No comments