BENKI YA DUNIA YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI MRADI WA EASTRIP DIT
Na Mwandishi Wetu.
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini Victoria Kwakwa ameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa utekelezaji unaoridhisha wa mradi wa Kujenga Ujuzi na Ushirikiano Afrika Mashariki (EASTRIP) unaotekelezwa na nchi tatu za Afrika Mashariki—Tanzania, Kenya, na Ethiopia kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia.
Ametoa pongezi hizo alipotembelea DIT akiongozana na mwenyeji wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda kukagua miradi ya EASTRIP inayotekelezwa chuoni hapo ikiwa ni pamoja na Jengo la Umahiri wa Tehama lenye uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 2000 kwa wakati mmoja.
Kwa Upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kufadhili miradi ya Elimu kuanzia Elimu Msingi (BOOST), Elimu ya Sekondari (SEQUIP) Mradi wa Kuongeza Umahiri wa TEHAMA (EASTRIP) hadi Elimu ya Juu (HEET).
"Kwa sasa tunafurahi kwasababu Benki ya dunia inatusikiliza nchi inataka nini, na Serikali yetu inataka nini halafu wanaungana na sisi kuhakikisha wanafanikisha kile ambacho tunakitaka"
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Mhandisi Dkt. Richard Masika amesema mradi wa EASTRIP unaleta mageuzi makubwa kwa wanafunzi kwa kuwajengea uwezo wa kuunganisha nadharia na vitendo ili kupunguza pengo lililopo kati ya yanayofanyika katika Taasisi za Teknolojia na kilichopo kwenye ulimwengu wa Viwanda.
Aidha Dkt. Masika amebainisha DIT inaendelea kuendeleza na kulea ujuzi wa wanafunzi kupitia kituo chake,
"kuna kituo ambacho kinawasaidia wanafunzi bunifu zao. Wanapata fursa ya kupaki hapa chuoni (DIT) na kuendeleza zile bunifu zao ambazo zinauwezekano wa kuingia sokoni kwa maana ya kwamba kuziwezesha kufikia ngazi hiyo ya kwenda sokoni kiasi cha kupelekea kwamba wao wanaweza wakaanzisha kampuni zao wenyewe na wakajitegemea"
Kupitia utekelezaji wa mradi wa EASTRIP Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imeweza kuongeza udahili wa wanafunzi, hususan kwa kuongeza asilimia 25 ya udahili wa wanafunzi wa kike katika masomo ya sayansi na teknolojia.
Kwa ujumla, EASTRIP inalenga kuboresha ujuzi na kuongeza ushindani wa kikanda katika sekta za kipaumbele, hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu ya nchi zinazoshiriki.
Post Comment
No comments