Breaking News

WANAFUNZI 30 DIT WAPATA FURSA YA KWENDA KUSOMA CHINA KUONGEZA UJUZI

 Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda leo ameshiriki hafla fupi ya Kuwaaga Wanafunzi 30 wa Taasisi ya Teknolojia  ya Dar es Salaam (DIT) wa Shahada ya kwanza ya Uhandisi Ujenzi  wanaotarajia Kwenda nchini China kuendelea na Mafunzo yao ya Mwaka wa pili na wa tatu.

Programu hii inatokana na makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya Elimu baina ya Taasisi  ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Taasisi ya Chongqing (CQVIE) ya nchini China yaliyofanyika tarehe 1/12/2022.

Akizungumza Katika hafla  hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ASA Prof Mkenda ambae pia alikuwa Mgeni Rasmi amewataka Wanafunzi hao kutumia nafasi hii adhimu kujifunza zaidi kutoka kwa wachina ambao Teknolojia yao  ipo juu sana kulinganisha na nchi zingine ikiwemo Tanzania.

Mkenda ameelezea furaha aliyonayo mbele ya Mwakilishi  wa Balozi  wa China nchini Tanzania  Che Zhao Guang kufuatia mafanikio haya ya kuwapeleka Wanafunzi nchini China kwa kuwa adhima hii inaunga mkono jitihada za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuwapatia Wanafunzi ujuzi wa kutosha utakaowasaidia kujipatia ajira ama kujiajili wao wenyewe.


Aidha, Waziri Mkenda amesema, japo katika hatua hii ya kwanza idadi ya Wanafunzi wanaokwenda ndogo sana ataendeelea kutafuta fursa nyingi Zaidi.

"Ninafarijika sana japo kuwa idadi inayokwenda tunaweza kuona ni wachache lakini jamani hata mbuyu ulianza kama mchicha kwa hiyo huu ni mwanzo mzuri tumeanza naamini inavyoendelea tutapeleka vijana wengi zaidi kwa kuwa lengo letu ni kupata wataalam wabobezi"amesema Mkenda.

Hata hivyo Prof. Mkenda mbali na kuwapongeza Wanafunzi  hao amewaasa kusoma kwa bidii, kutunza tamaduni za kitanzania ameiomba pia Serikali ya China kuendelea kutoa fursa ya ufadhili mkubwa ili kuweza kupeleka wanafunzi wengi zaidi.

No comments